Na Beatrice Lyimo-Maelezo-Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Annastazia Wambura anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi katika Tamasha la Sanaa litakalofanyika Septemba 24, mwaka huu
katika kijiji cha Makumbusho Jijini Dar salaam.
Tamasha hilo ni sehemu ya
maandalizi ya matamasha yanayofanyika katika kuelekea maadhimisho ya
kilele cha Siku ya Msanii Tanzania inayotarajiwa kufanyika Octoba 29
mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Haak Neel Production Bw.
Godfrey Mahendeka alisema kuwa lengo la tamasha hilo ni kutambua,
kuhamasisha na kuthamini kazi na machango unaotolewa na wasanii nchini.
Amesema kuwa Tamasha hilo
litawakutanisha wasanii wa aina zote ikiwemo Sanaa za muziki, filamu,
ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa hadhira.
“Kwa mara ya kwanza tamasha
hili linawakutanisha wasanii aina zote kwenye eneo moja yaani sanaa za
muziki, filamu, ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa
hadhira” alifafanua Bw. Mahendeka.
Aidha, aliongeza kuwa tamasha
hilo litapambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo huduma ya uchangiaji
damu, elimu ya mifuko ya jamii kwa wasanii na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake mwakilishi
kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Bw. Augustino Makame aliwataka
wasanii wa fani zote kujitokeza kwa wingi kwani siku hiyo ni fusra ya
wasanii hao kubadilishana mawazo na uzoefu walionao.
Naye Msanii wa Bongo Fleva na
mmoja wa wasanii watakaoshiriki tamasha hilo Bw. Peter Msechu
ameipongeza Serikali kwa kuwajali wasanii na kupelekea kuundwa kwa idara
itakayoshughulikia masuala ya sanaa.
Hata hivyo, Msanii huyo ametoa
wito kwa Serikali kuzidi kufuatilia kazi za wasanii na kuzuia kuingiza
kazi za wasanii ambazo hazijajkidhi vigezo zinazotoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment