Saturday, 18 February 2017

Wakurugenzi wa halimashauri wameaswa kutumia fursa uwepo wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo

1
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) akiwasili Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi mwishoni wa wiki kujionea namna chuo hicho kinavyoendesha programu zake katika jitihada za kuendeleza sekta ya michezo nchini. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa chuo Richard Mganga na wa kwanza kulia ni Rais wa Serikali ya wananchuo Cletus Mutakyawa.
2
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa nne kushoto aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi mwishoni wa wiki kujionea namna chuo hicho kinavyoendesha programu zake katika jitihada za kuendeleza sekta ya michezo nchini. 

Na Eleuteri Mangi, WHUSM 18/02/2017
Wakurugenzi wa halimashauri wameaswa kutumia fursa uwepo wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo mkoani Mwanza kwa kuwaruhusu walimu wa michezo wengi zaidi kuongeza ujuzi wao ili kuinua sekta ya michezo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea chuo hicho kujionea namna chuo hicho kinavyoendesha programu zake katika jitihada za kuendeleza sekta ya michezo nchini.
 “Nawapongeza viongozi, wafanyakazi na wanachuo kwa juhudi mnazofanya katika kukiimarisha chuo hiki ambacho ni hazina ya michezo mbalimbali nchini, mmepiga hatua kubwa ya kimaendeleo” alisema Prof. Ole Gabriel.
Chuo hicho kimekuwa msingi wa kujenga wataalam wa michezo nchini kwa lengo la kuimarisha mahusiano na maendeleo ya kielimu kijamii, kielimu, kikazi na kiuchumi kwa kuzishirikisha halmashauri zote nchini.
Katika kuenedeleza michezo nchini, Prof. Ole Gabriel amewaambia viongozi wa chuo hicho kuwa wawe wabunifu kwa kuongeza programu nyingi zaidi chuoni hapo ambazo zitaongeza kipato na tija kwa chuo, wanachuo, wananchi wanazunguka chuo na taifa kwa ujumla.
Aidha, Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa ni vema chuo hicho wapange na kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ili kurahisishs watu kupata elimu ya michezo na kuongeza tija katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo Richard Mganga akitoa taarifa yake kwa Katibu Mkuu mwenye dhamana ya michezo Prof. Ole Gabriel alisema kuwa chuo hicho kimepata Ithibati kamili mwaka 2015 na kinafundisha kozi ambazo zinafuata mitaala iliyopitishwa na Baraza la Taifa La Elimu ya Ufundi (NACTE).
 
Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza chuo kimekuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili kwa kozi za Stashahada ya Utawala na Uongozi katika Michezo, Stashahada ya Elimu ya Michezo, Stashahada ya Ukocha tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na wanafunzi mwaka moja tu.
Hali hiyo imefanya idadi ya wanachuo mwaka huu wa masomo 2016/2017 kuongezeka ambapo hadi sasa wapo wanachuo 99 ambapo mwaka wa kwanza idadi yao ni 46 na mwaka wa pili wakiwa 53.

No comments:

Post a Comment