Thursday, 23 February 2017

Chama cha Kuogelea nchini Tanzania (TSA) kimeteua wachezaji wawili watakaoshiriki mashindano ya vijana ya Jumuiya ya Madola

1
    Celina Itatiro katika mashindano ya kuogelea ya Tanzania
2
 Collins Saliboko (katikati) mara baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Tanzania. Collins kwa sasa yupo masomoni, London
 Celina Itatiro akishindana kwenye mashindano ya Afrika Kusini
4
  Celina Itatiro katika staili ya backstroke.
Na Mwandishi wetu
Chama cha Kuogelea nchini Tanzania (TSA) kimeteua wachezaji wawili watakaoshiriki mashindano ya vijana ya Jumuiya ya Madola yaliyopangwa kufanyika mjini Nassau, Bahamas kuanzia Julai 18 mpaka 23 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhan Namkoveka aliwataja wachezaji hao kuwa ni Celina Itatiro anayetokea klabu ya Dar Swim Club na Collins Saliboko ambaye  ni mwanafunzi wa Shule ya St Felix iliyoko Uingereza.
Namkoveka alisema kuwa wachezaji hao wamepata nafasi hiyo baada ya kuwa na muda mzuri kulinganisha na wengine (Personal Best) na hivyo kuchaguliwa kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ya sita.
Alisema kuwa wameamua kuwatangaza mapema ili kuwawezesha kujiandaa vilivyo kwani lengo la TSA ni kuona watanzania wanafanya vizuri katika mashindano hayo na kuongeza nafasi ya nchi kufuzu katika mashindano ya Olimpiki ya 2020 yaliyopangwa kufanyika mjini Tokyo, Japan.
Alisema kuwa Celina ana muda mzuri kwa upande wa wasichana na ana uzoefu wa kimataifa kutokana na kushindana katika mashindano mengi ya ndani na nje ya nchi.
 
“Collins ni mmoja wa wachezaji walioko katika shule ya St Felix ambao wanasoma na pia wanafanya mazoezi ya hali ya juu ili kuweza kulinda na kuimarisha viwango vyao vya muda wa kuogelea. Hivyo naye ni mmoja wa waogeleaji tegemezi wa Tanzania,” alisema Namkoveka.
Alifafanua kuwa  kazi iliyopo sasa ni kwa makocha kuwaandaa wachezaji katika matukio watakaoshiriki ili kuweza kufanya vizuri hasa lengo kuu la chama la kuwa na wachezaji wanaopunguza muda yao ili baadae waweze kufikia muda unaotakiwa na FINA wa kiwango cha muda B au A.
Namkoveka ameishukuru kamati ya Olimpiki Tanzania kwa kuweza kuteua chama cha Kuogelea kushiriki mashindano hayo.
“Hii ni faraja sana kwa wana familia wa mchezo wa kuogelea, uteuzi huu utasaidia sana juhudi za chama za kuweza kuhakikisha inakuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa na wakiwa muda mzuri zaidi wa kuweza kufuzu mashindano ya Olimpiki ya 2020,” alisema.
Mashindano ya jumuiya ya madola haya yatakuwa ya sita baada ya kuanzishwa kwake mwaka 2000 na wakitegemewa vijana 1000 wenye  umri wa miaka kuazia maika 14 hadi 18  kushindana katika michezo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment