Na Lydia Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inatarajia
kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya Mahakama
katika kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya utoaji
haki kwa wananchi.
Ili kusogeza huduma hiyo kwa
wananchi, majengo ya Mahakama kuu katika mikoa tisa yanatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha miaka miwili, Mahakama za Mikoa sita
zitajengwa ndani ya miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo
36 zinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho
ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika hivi karibuni, Kaimu Jaji Mkuu
wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma alisema Mahakama kwa kushirikiana na
Wakala wa Majengo (TBA), Chuo Kikuu cha Ardhi, Baraza la Ujenzi la
Taifa, Benki ya Dunia na wadau wengine wanaendeleza na kukamilisha
miradi ya ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa tisa nchini.
Aliitaja mikoa ambayo majengo ya
Mahakama Kuu yatafanyiwa ukarabati na mengine kujengwa ndani ya kipindi
cha miezi 24 kuwa ni Mbeya, Kigoma, Mara, Tanga na Dar es salaam. Mikoa
mingine ni Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma.
Alisema nia ya Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa ili kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi.
“Tunapaswa kuwa na Mahakama Kuu
26 kwenye kila ngazi ya Mkoa, kwa sasa tunazo Mahakama Kuu kwenye kanda
14 tu”, alisema Kaimu Jaji Mkuu.
Aidha, mikoa 12 isiyokuwa na
Mahakama Kuu ni pamoja na Songwe, Katavi, Njombe, Lindi, Kigoma na Mara.
Mikoa mingine ni Singida, Morogoro, Pwani, Simiyu, Geita na Manyara.
Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa
wakati huo huo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha ujenzi wa
Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa sita ya Manyara, Geita, Simiyu,
Njombe, Katavi na Lindi katika kipindi cha kati ya miezi 6 na mwaka
mmoja.
Kwa upande wa Mahakama za Wilaya
na zile za Mwanzo, Kaimu Jaji Mkuu alisema wanakusudia kujenga Mahakama
za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 ambazo zitakamilika ifikapo Desemba 2017.
Alisema hatua hii ya ujenzi wa
Mahakama hizi si tu kwamba itasogeza karibu huduma za Mahakama kwa
wananchi bali pia italeta mabadiliko makubwa ya miundombinu ya mahakama
na kuweka historia ya upatikana wa miundombinu kwa wingi na kwa kifundi
kifupi.
No comments:
Post a Comment