Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pamoja na mambo mengine ina jukumu la
kusimamia na kuratibu ajira za wageni nchini. Hii inajumuisha kupokea na
kushughulikia maombi ya vibali vya kufanya kazi nchini kwa wageni na
kutoa vibali husika.
Katika kipindi cha hivi karibuni
imebainika kwamba kuna baadhi ya waajiri na wageni kwa kujua ama kwa
kutokujua wanakiuka masharti yaliyoainishwa na Sheria ya Kuratibu Ajira
za wageni Na. 1/2015. Tabia hii imekuwa ikifanywa na baadhi ya waajiri
na madalali wanaowatumia.
Ofisi inawajulisha waajiri wote
kwamba, mfanyakazi wa Kigeni kufanya kazi bila kibali cha kazi
kilichotolewa na Kamishna wa Kazi ni kosa la jinai. Hivyo, waajiri wote
wanapaswa kuzingatia kuwa wafanyakazi wao wa kigeni wanakuwa na vibali
halali vya kazi.
Ofisi inawajulisha waajiri kwamba
kutakuwa na ukaguzi maalumu wa kuhakiki vibali vya kufanya kazi nchini
ili kuhakikisha kuwa wageni wote wanaofanya kazi wana vibali halali vya
kazi. Hivyo, wageni wote wanaofanya kazi nchini wanapaswa kuwasilisha
vibali vyao katika Ofisi za Kazi za kila Mkoa kwa ajili ya uhakiki ndani
ya siku 30 toka tarehe ya tangazo hili.
Kamishna wa Kazi anatoa rai kwa
waajiri na wageni wote wanaofanya kazi nchini kushiriki kikamilifu
katika zoezi hili la kuhakiki vibali ili kuepuka usumbufu wowote usio wa
lazima.
Imetolewa na;
KAMISHNA WA KAZI
OFISI YA WAZIRI MKUU
KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU
22/02/2017
No comments:
Post a Comment