Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Nile “Nile Day” yatakayofanyika wiki ijayo (Februari, 22), jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na
Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na taasisi inayosimamia
shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile-Nile Basin Initiative (NBI).
Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mha. Gerson Lwenge ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiongea na
mwandishi wa habari hii kuhusu maadhimisho hayo.
Mha. Lwenge amesema kuwa
maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka miongoni mwa nchi wanachama 10
zilizo katika bonde la mto huo; ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan,
Sudan ya Kusini na Misri, ambapo kwa mwaka huu siku hiyo inasherekewa
nchini Tanzania.
“Lengo la Siku ya Nile ni kukuza
uelewa kwa watu wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote
wanachama, masuala yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na
matumizi bora ya rasilimali za Bonde la Mto Nile,” alisema Mha. Lwenge.
Amefafanua kuwa maadhimisho hayo
yatasaidia kufahamu zaidi kuhusu umuhimu wa mto huo katika kutupatia
chakula cha uhakika, maji, nishati ya umeme na faida nyingi kiuchumi
pamoja na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kulinda na kutumia rasilimali
za mto huo kwa pamoja na kwa usawa na uendelevu kwa ajili ya kizazi cha
leo na vizazi vijavyo.
Mha. Lwenge ameongeza kuwa
maadhimisho hayo yataambatana na maandamano kutoka viwanja vya Mnazi
Mmoja mpaka Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, upandaji
wa miti, maonesho ya vitu mbalimbali vinavyohusu Sekta za Maji na
Umwagiliaji, burudani za kiutamaduni, pamoja na za watoto wa shule za
msingi na sekondari.
Aidha, Waziri Lwenge amewataja
washiriki wa maadhimisho hayo kuwa ni mawaziri wanaohusika na maji
kutoka nchi wanachama, mabalozi, wawakilishi kutoka NBI, wabunge,
washirika wa maendeleo, wataalamu, wanafunzi wa vyuo, sekondari na shule
za msingi, taasisi binafsi, vyombo vya habari pamoja na umma kwa
ujumla.
NBI ilianzishwa rasmi mwaka 1999,
jijini Dar es Salaam, ambapo nchi wanachama waliungana na kukubaliana
kuanzisha umoja wa ushirikiano katika kusimamia na kuendeleza rasilimali
za Bonde la Mto Nile.
No comments:
Post a Comment