Monday, 27 February 2017

Mhe Job Ndugai amewaahidi Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali

1
Spika wa Bunge  Mhe Job Ndugai akizungumza na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Skauti waliomtembelea Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam mapema leo. Wa pili  kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Eng. Stella Manyanya (Mb) na anayefutia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Skauti Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga.
2
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Eng. Stella Manyanya (Mb) aliyeambatana na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Skauti Tanzania akimueleza jambo Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai wakati walipotembelea Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
3
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Skauti Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga akimueleza jambo Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai wakati walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
4
Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai (aliyekaa kulia) na  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Eng. Stella Manyanya (Mb) katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Skauti Tanzania mara baada ya kuzungumza nao Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Picha na Ofisi ya Bunge
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   Mhe Job Ndugai amewaahidi Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama hicho ikiwemo maadhimisho ya Siku ya Skauti Afrika na Maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini.
Mhe Spika aliyasema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na  Viongozi wa Kamati ya Utendaji ya Skauti Tanzania  Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam ambao walimuomba awaunge mkono katika shughuli zao.
Spika Ndugai aliwaeleza Viongozi hao kwamba kwa niaba ya Wabunge wote ameupokea ujumbe huo na atajitahidi sana katika kuhufikisha kwa Waheshimiwa Wabunge.
“Ninawashukuru sana kwa ujumbe huu na niwaahidi kwamba tupo pamoja si katika hili tu bali katika mambo yoyote ambayo mtakuwa mkiyafanya na nawaahidi pia ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge katika maadhimkisho hayo,” alisema Mhe Spika.
Awali akimuelezea Mhe Spika kuhusiana na Shughuli mbalimbali za Skauti hapa nchini Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Stella Manyanya ambaye aliambatana na Viongozi hao wa Skauti alisema pamoja na majukumu mengine Chama hicho cha Skauti kina kazi kubwa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya Skauti Dunia na Maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini.
Mhe Manyanya alisema   kuwa maandalizi ya  Maadhimisho ya siku Skauti Afrika ambayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 8 hadi 11 Machi mwaka huu mkoani Arusha yanaendelea vizuri ingawa kuna changamoto kubwa ya kifedha katika maandalizi ya maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni hadi Julai Mkoani Dodoma.
“Mhe Spika kumekuwa na jitihada mbalimbali za kufanikisha maadhimisho haya lakini kumekuwa na changamoto katika kufikia malengo na ndio maana tumefikana hapa ili kukuomba utuunge mkono” alisema Mhe Manyanya.
 
Mhe Manyanya aliongeza kuwa Wizara imendelea kutambaua kazi kubwa ambayo Chama cha Skauti inafanya katika kuendelea kuhimiza nidhamu miongoni mwa Vijana na kuwajengea moyo wa kujitolea.
“Chama hiki Mhe Spika kimekuwa kikiendelea kufanya kazi kubwa katika kuwajengea Vijana wetu moyo wa kujitolea na kwa sasa tunataka kazi zao zifanyike kwa nguvu zaidi tofauti na hapo mwanzo”
Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Skauti Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga alisema anathamini sana mchango wa Mhe Spika na kwamba anashukuru kwa kauli yake ya kuwaunga mkono.
Balozi Kuhanga aliongeza kuwa kwa sasa Uongozi wake unajipanga katika kuhakikisha kuwa Skauti inazidi kukua hapa nchini.
“Mhe Spika nia ni kuona Vijana wa Shule za Msingi hadi Chuo Kikuu wanaingia katika Skauti na hivyo tunataka twende mbele zaidi ya hapa tulipo kwa sasa,” alisema Balozi Kuhanga.

No comments:

Post a Comment