Na. Immaculate Makilika na Lilian Lundo- MAELEZO.
.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni ametoa wito wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini Uganda.
Rais Museveni ametoa kauli hiyo
leo wakati alipotembelea viwanda vya Kampuni ya Bakhresa vinavyozalisha
Unga na Juisi vya Buguruni na Vingunguti jijini Dar es Salaam.
“Nawakaribisha wafanyabiashara wa
Kitanzania kuja nchini Uganda kuwekeza kwani kufanya hivyo kutasaidia
kuzalisha bidhaa, upatikanaji wa soko pamoja na ajira” alisema Rais
Museveni.
Kauli hiyo ya Rais Museveni
imetokana na mafanikio yanayotokana na Mwekezaji wa Kitanzania Said
Salim Bakhresa aliyewekeza nchini Uganda ambapo anamiliki Kiwanda cha
kusanga ngano nchini humo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa
Mahusiano wa Kampuni za Bakhresa Hussin Sufiani amesema kwamba Kampuni
hiyo iko mbioni kuongeza uzalishaji wa unga wa ngano kutoka tani 1,100
hadi kufikia tani 2,000 kwa siku nchini Uganda.
Aidha, amesema kutokana na
uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Uganda jumla ya Waganda 650 wamenufaika
na ajira mbalimbali ambazo zinasaidia kuwapatia kipato.
Kwa upande wa Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwaijage amesema kuwa Uganda na
Tanzania zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali
ikiwemo sekta ya viwanda.
Amesisitiza Watanzania wanaweza
kwenda kuwekeza nchini Uganda kwa vile nchi hiyo wanalima tani milioni 4
za mahindi lakini wana uwezo wa kutumia tani milioni moja pekee, hivyo
ni fursa kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini humo.
“Tunawahamasisha wafanyabiashara
wa Uganda na Tanzania kuwekeza katika nchi zao ili kuzalisha , bidhaa na
ajira za kutosha kwa wananchi” alisema Waziri Mwijage.
Waziri Mwijage alitoa Wito kwa
Watanzania kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kufanya uzalishaji wa
bidhaa zinazotumika viwanda mfanio kwa kulima matunda au mbogamboga.
Rais Yoweri Museveni aliwasili
nchini jana kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili ambapo akiwa nchini
alifanya mazungumzo na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kutembelea Viwanda vya Said
Salim Bakhresa vya Tazara na Vingunguti.
No comments:
Post a Comment