Kada wa Chama cha Mapinduzi na
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, wilaya ya Kati,Mkoa wa Kusini Unguja
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es
Salaam, kuhusu kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika vita dhidi ya
dawa za kulevya nchini.
Kada wa Chama cha Mapinduzi na
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, wilaya ya Kati,Mkoa wa Kusini Unguja
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari –
MAELEZO leo Jijini Dar es Salaam, kuhusu kuunga mkono juhudi za Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt. John Pombe
Magufuli katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO.
Na. Lilian Lundo – MAELEZO
Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Mohammed
Raza ameunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya inayoendeshwa na
Serikali ya Awamu ya Tano.
Raza ameyasema hayo leo, Mjini
Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari juu ya vita hiyo
ya dawa za kulevya inayoendelea nchini.
“Naunga mkono juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni
imani yangu vita hii dhidi ya dawa za kulevya tutaishinda, kama
tulivyomshinda nduli Idd Amini,” alifafanua Raza.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kila
Mtanzania anatakiwa kuwa na uchungu na nchi yake kwa kuunga mkono vita
dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwa biashara hiyo inadhoofisha nguvu ya
Taifa.
Aidha amesema kuwa dawa za
kulevya ni janga la Dunia nzima na uwezo wa kuliondosha kwa Tanzania
unahitaji ushirikiano wa Serikali zote mbili za Tanzania Bara na
Visiwani na wananchi wake.
Hata hivyo, Raza ameiomba
Serikali kununua vifaa vya kisasa vitakavyosaidia kutambua dawa za
kulevya ili kuzuia uingizaji wa dawa hizo hapa nchini, hasa kwa Zanzibar
ambayo imezungukwa na bahari hivyo kurahisisha uingizaji kutokana na
kutokuwepo kwa vifaa hivyo.
Katika hatua nyingine Raza
amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kurejesha maadili kwa watanzania na
viongozi tofauti na ilivyokuwa hapo zamani.
Amesema kuwa haikuwa rahisi kwa
mtoto wa mkulima kupata ajira lakini kwa Serikali Awamu hii watanzania
wote wamekuwa na thamani bila kubaguliwa kutokana na kipato, rangi,
kabila au dini zao.
No comments:
Post a Comment