Thursday, 2 February 2017

Aishi bila mapafu kwa siku sita


Maisha ya mwanamke raia wa Canada, yameokolewa katika upasuaji wa aina yake ulioambatana na madaktari kuondoa mapafu ndani ya mwili wake kwa siku sita, wakati akisubiri kumfanyia upasuaji wa kumpandikizia mapafu mengine.
Mwanamke huyo, Melissa Benoit (32), aliyezaliwa akiwa na ugonjwa wa kurithi unaoathiri tezi, alikuwa na maambukizi makali ya bakteria kwenye mapafu yake.
Alikuwa na hali mbaya wakati alipolazwa kwenye hospitali kuu iliyoko jijini Toronto.
Ulikuwa upasuaji wa aina yake, kwani mapafu yake yote yalitolewa nje na baadaye kuwekewa pafu moja dogo la kuhamishwa, ambalo liliungwanishwa na moyo.
Timu ya wataalamu 13 wa upasuaji, wakiwamo mabingwa watatu wa upasuaji wa kifua, walishiriki katika juhudi za kuondoa viungo vya mama huyo.
Shughuli hiyo ya upasuaji ilichukua muda wa saa tisa.
Hatari zilizoambatana na shughuli hiyo ya upasuaji zilijumlisha kumwagika kwa damu ndani ya kifua kilichokuwa wazi, uwapo wa shinikizo la damu, kiwango cha oksijeni ambacho hata hivyo kingeweza kusaidiwa baadaye na kama angeweza kuishi kutokana na upasuaji huo.
Baada ya mapafu yake kuondolewa, hali ya Benoit ilitengemaa na mapafu mengine kutoka kwa mfadhili yalipatikana baada ya siku sita baadaye, ambapo ndipo alipoweza kupandikizwa mapafu hayo mengine.

Mwanamke huyo, mama wa mtoto mmoja alisema:
“Kupandikiziwa mapafu haya mengine, ndiko kulikookoa maisha yangu, kwani kama nisingeyapata ningeweza kufa,” anasema na kuongeza:
“Nisingekuwapo hapa kumuona binti yangu akikua na kufikia utu uzima, akiolewa na kuwa na mumewe. Hilo ni moja ya mambo ninayoyahitaji sana katika maisha yangu. Kwa kweli nilikuwa hatarini kuvikosa.”

Kwa upande wake, bingwa wa upasuaji Dk. Shaf Keshavjee anasema:“Huu ulikuwa upasuaji mgumu na wenye changamoto nyingi. Melissa alikuwa anakufa mbele yetu.”
Anaongeza: “Tulipaswa kufanya maamuzi, kwa sababu bila hivyo, Melisa alikuwa anakufa usiku huo. Yeye ndiye aliyetutia moyo wa kusonga mbele.”

Kimsingi, ni upasuaji mkubwa na uliofanyika kwa mafanikio makubwa sana katika historia ya upasuaji, si tu kwa Canada, bali dunia nzima.
Familia yake ilisema, mama huyo kila mara aliwaambia kuwa katika suala lake la kusaka tiba, angependa ajaribu kila kitu kinachowezekana, ili aweze kuishi kwa ajili ya mumewe Christopher na binti yake Olivia, mwenye umri wa miaka miwili.
Naye Dk. Marcelo Cypel, daktari bingwa wa upasuaji wa kifua anasema kuwa mapafu yake mapya yanafanya kazi vizuri na yaliingizwa kwa urahisi.

No comments:

Post a Comment