Dodoma, Alhamisi, 2 Februari, 2017:
Serikali imetoa ufafanzi
kuhusu masuala mbalimbali kuhusu utawala wa Sheria na kuainisha mikakati
yake katika kuzuia au kupunguza athari za matetemeko ya ardhi nchini.
Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo.
Serikali Kutoingilia Mihimili ya Dola
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu mgawanyo wa mihimili mitatu ya dola
nchini. Waziri Mkuu alikuwa akifafanua kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya
wafuasi wa vyama vya siasa kesi zao zinachukua muda mrefu.
Aidha, Waziri Mkuu amekanusha
vikali madai kuwa Serikali inakusudia au imetangaza kufuta vyama vya
siasa hasa vya upinzani nchini madai yaliyotolewa na Kiongozi wa
Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe.
Mkakati Kuzuia Majanga Ya Asili
Akijibu hoja kuhusu mikakati
ya kupambana na athari za majanga ya asili, Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde, amesema Serikali
tayari inao mkakati wa kitaifa wa kupambana na majanga ya asili yakiwemo
matetemeko.
Aidha, Serikali imeandaa Sera
ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo imeainisha aina mbalimbali za
maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na majukumu ya kila mdau katika
kushughulikia maafa. Aliongeza kuwa, Serikali pia imeandaa Mwongozo wa
Taifa wa Kukabiliana na Maafa ambao unaelekeza Taasisi kiongozi na
wajibu wao wakati wa kukabiliana na majanga.
Liganga, Mchuchuma Kuzalisha Megawati 350
Serikali imesema kuwa, miradi
unganishi ya Mchuchuma na Liganga itakayotekelezwa kati ya Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Group (SHG)
Limited ya China kupitia ubia wa pamoja wa Tanzania China International
Mineral Resources Limited (TCIMRL) itazalisha zaidi ya ajira 33,000 na
kuipatia nchi umeme wa megawati 350.
Akitoa ufafanuzi huo, Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa kampuni
hiyo imeshapewa leseni na vibali vingine muhimu na sasa inakamilisha
ulipaji wa fidia ili kuanza kazi. “Miradi hiyo unganishi itawezesha
kuchimbwa makaa ya mawe kiasi cha tani milioni (3) na chuma ghafi tani
milioni 2.9 kwa mwaka,” alisema.
Usalama wa Raia Mipakani
Serikali kupitia vyombo vya
ulinzi na usalama katika maeneo ya mipaka inachukua hatua za pamoja na
vyombo vya nchi jirani kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao
katika maeneo hayo.
Akijibu hoja kuhusu suala la
usalama wa raia wanaoishi pembezoni mwa mipaka ya Tanzania, Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amefafanua kuwa
operesheni za pamoja zinafanyika katika mipaka ya nchi na vikao vya
ujirani mwema ili kuhakikisha usalama. Wananchi wameombwa kutoa taarifa
wanapowaona wageni wasioeleweka katika maeneo yao ili kuimarisha
usalama.
Wanahabari Waendeleze Kiswahili
Serikali imewapa changamoto
wanahabari nchini kuwa chachu ya kuendeleza lugha ya Kiswahili. Wakijibu
maswali mbalimbali ya wabunge kuhusu matumizi ya Kiswahili fasaha
katika vyombo vya habari, Waziri na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, wameliambia Bunge kuwa, ni vyema sasa hata wamiliki wa
vyombo vya habari wakaanza kuzingatia ufaulu kwa somo la Kiswahili
kabla ya kuwaajiri waandishi.
Kwa upande wake Waziri Nape
akitoa majibu ya nyongeza, alisema kuenziwa kwa Kiswahili nchini kumeipa
Tanzania hadhi ya kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za Afrika
zinazojihusisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment