MJUMBE
mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ali Mzee (katikati), akipanda mti
katika zoezi la upandaji miti lililofanyika uwanja wa michezo Malindi
mjini Zanzibar jana, kwa lengo la kuhuisha mandhari ya eneo hilo ambalo
limeanza kuathiriwa na athari za kimazingira. Kushoto ni Mwenyekiti wa
jumuiya ya Green World Family Foundation iliyodhamini zoezi hilo Nazir
Ahmad Bachoo iliyodhamini shughuli hiyo. (Picha na Haroub Hussein).
Na Salum Vuai, MAELEZO
JAMII nchini imehimizwa kujenga
utamaduni wa kupanda miti ili kuirejeshea Zanzibar uoto wa asili na
kuiepusha na janga la kimazingira.
Akizindua zoezi la upandaji miti
lililofanyika pembezoni mwa uwanja wa soka wa klabu ya Malindi mjini
Zanzibar, mjumbe mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Ali Mzee, amesema miti
ni uhai kwa kila binadamu.
Mzee alisema ni jambo la
kusikitisha kwamba mazingira ya Zanzibar yamegeuka kutoka rangi ya
kijani iliyokuwepo zamani na kuwa yabisi, hali inayosababisha kuongezeka
kwa joto.
“Bila miti, viumbe hutaabika na
nchi inakuwa kavu na maradhi hasa presha huongezeka kila uchao. Lazima
tuzinduke kwani tusipopanda miti, tunakaribisha janga kwa taifa,”
alisema Mzee.
Aidha alivitaka vyombo vya habari
kuandaa vipindi na makala mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa
wananchi juu ya umuhimu wa kupanda miti.
Mapema, Mwenyekiti wa jumuiya ya
Green World Family Foundation iliyodhamini zoezi hilo Nazir Ahmad
Bachoo, alisema jumuiya yake inathamini mazingira na imeamua kulifanya
zoezi la upandaji miti kuwa endelevu.
Alisema ni jambo lililo wazi
kwamba dunia nzima sasa inalia na hali ya joto litokanalo na ongezeko la
hewa ukaa (carbon dioxide), inayosababishwa na upungufu wa miti na
kuongezeka kwa vyombo vya usafiri barabarani vinavyozalisha moshi kwa
wingi.
“Umefika wakati sasa kila mmoja
ahamasike kupanda na kuitunza miti katika eneo analoishi na yale
yanayomzunguka, ili ilete manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, mratibu wa zoezi
hilo na mwanaharakati wa mazingira Mohammed Abdulrahman Bajbeir,
alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na wataalamu wengi wa masuala ya
mazingira, lakini bado hawajatumika kikamilifu kuisaidia nchi.
Kwa hivyo amezishauri mamlaka za
juu kutanabahi na janga la kimazingira linaloinyemelea Zanzibar kutokana
na utashi wa binadamu ambao wamekuwa wakikata miti ovyo bila kupanda
mingine.
“Zanzibar ya sasa sio kama ile ya
zamani ambayo ilijaa kila aina ya miti pembezoni mwa barabara na
mitaani. Tunafyeka miti kujenga nyumba za makaazi na maduka tukisahau
kwamba miti ni muhimu kwa uhai wetu. Tubadilike,” alieleza Bajbeir.
Wananchi mbalimbali wa mitaa ya
Malindi, Mchangani na Mbuyuni wakiwemo wanasoka wa zamani wa klabu ya
Malindi SC walioshiriki zoezi hilo, walieleza umuhimu wa kuilinda miti
hiyo ili kuunusuru uwanja wa michezo, kwani umekuwa ukiharibiwa sana na
watu wanaoweka magari pamoja na mifugo.
Jumla ya miti 41 ya aina
mbalimbali ilipandwa kuzunguka uwanja huo, na itakuwa ikilindwa na
wananchi kwa kushirikiana na vijana wa ulinzi shirikishi na polisi jamii
wa shehia ya Malindi.
No comments:
Post a Comment