watu wakisaidia kutoa mizigo kwenye meli ya kampuni ya New Happy
baada ya kuzama katika bahari ya Hindi wakati ikitoka Dar es Salaam
kuelekea Zanzibari jana. Picha na Salma Said
Na Mwandishi Wetu
Meli hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara mashuhuri wa vyombo vya usafiri wa baharini nchini, Khamis Kipara ilizama bahari ya Hindi wakati ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Zanzibar.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam alisema meli hiyo ilianza kuzama saa 8:30 usiku wa kuamkia jana.
Mkadam alisema licha ya meli hiyo kukumbwa na mkasa huo usiku wa manane, taarifa za kuzama kwake zililifikia jeshi hilo saa mbili asubuhi jana.
“Chanzo cha ajali hiyo bado hatujakijua, tunaendelea na uchunguzi, ila mpaka sasa hakuna majeruhi wala maafa ya abiria yeyote yaliyoripotiwa kutokea meli hiyo”, alisema Mkadam.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mmoja wa mabaharia ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema; “siwezi kuelewa vyema tuko wangapi humu ndani ya meli lakini sidhani kuwa yupo aliyekosekana hadi sasa”.
Baharia huyo aliongeza; “pamoja na yote, huu ni msimu ambao mazingira ya baharini siyo rafiki sana kwa vyombo, abiria na hata mizigo kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa.”
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia kwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliyefika katika maeneo ya kupokelea na kufuatilia taarifa za meli hiyo, Maisara mjini hapa aliahidi kusaidia harakati za uokozi wa mali na mizigo.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza ambayo ni nadra kujitokeza Zanzibar, baadhi ya wananchi badala ya kusaidia kuokoa mali zilizozama katika ajali hiyo, walitumia fursa hiyo kujitosa majini na kujichukulia bidhaa walizofanikiwa kuokoa na kutokomea nazo.
“Ama kweli imani imekwisha na watu si binadamu tena,” alisema Salim Bakari (45). muuza samaki katika Bandari ya Kizingo ambaye alishuhudia meli hiyo ilivyokuwa ikizama baharini na pia watu walivyokuwa wakipigania mizigo hiyo.
Wafanyabiashara Rashid Said Juma na Ali Mohamed Said, wakazi wa Mlandege walikuwa walilalamikia kitendo cha kuchukuliwa mali zao na watu waliojitosa kuelekea meli hiyo ilipokuwa.
“Tulipata matumaini kuwa wale ni wasamaria wema walikuja kusaidia kutuokoa, kumbe ni kinyume chake, wengine walikuja kutuibia, balaa gani hili?” alihoji Mohamed.
No comments:
Post a Comment