Dar es Salaam. Mashabiki 40,000 wakiwamo 500 wa TP Mazembe watashuhudia mchezo leo wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Uwanja wa Taifa una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 kwa wakati mmoja, lakini kutokana na uamuzi wa viongozi wa Yanga kuwataka mashabiki kuingia bure CAF imeamua kupunguza idadi ya mashabiki kwa sababu za kiusalama.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema wameamua kuchukua uamuzi huo kufuatia ushauri uliotolewa na kamishnaa wa mchezo huo Celestine Ntangungira kutoka Rwanda.
“Tulipokutana na kamisaa alitumwambia mashabiki wataingia bure alitushauri kwa sababu za kiusalama mashabiki 40,000 pekee ndio waingie uwanjani. Pia tunatarajia kuwa na idadi ya polisi 500 ambao watalinda usalama muda wote wa mchezo,” alisema Muro na kuwataka mashabiki wa Yanga na Wwatanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia Yanga.
Mashabiki 500 wa TP Mazembe waliwasili nchini jana kwa mabasi wakitokea Lubumbashi kupitia Zambia, Tunduma hadi Dar es Salaam kuishangilia timu yao.
“Utaratibu umeandaliwa kwa ajili ya mashabiki wa TP Mazembe kuhakikisha wanapata sehemu nzuri ya kukaa na kuisapoti timu yao. Kiujumla maandalizi yote ya mchezo yamekamilika,” alisema Muro.
Ulinzi kwa CCTV
Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwahakikishia mashabiki usalama akisema Jeshi la Polisi litatumia kamera za CCTV kuimarisha usalama kwenye mchezo huo.
Kamanda Sirro alisema: “Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama tumejipanga kuhakikisha mechi hiyo inafanyika katika hali ya usalama.
“Sehemu zote za mageti ya kuingilia na kutokea na maeneo yote yatanaonekana na kuwekwa kumbukumbu za matukio ykwenyeatafungwa CCTV Camera, lakini pamoja na hayo wananchi wanatakiwa kuwa watulivu katika kushangilia mechi hiyo.
“Hawataruhusiwa kuingia uwanjani na chupa za kimiminika cha aina yeyote, silaha ya aina yoyote, kupaki magari ndani ya uwanja wala kukaa majukwaa ambayo hawapaswi kukaa,” alisema Kkamanda Sirro.
Serikali yaikaba TFF
Serikali imesema imeingia mkataba na Shirikisho la Soka (TFF) juu ya malipo ya uwanja hivyo mgao wao wa mapato ya mlangoni huko pale pale licha ya Yanga kutangaza mashabiki kuingia bure.
Waziri wa Michezo, Nape Nnauye alisema, wao wanaitambua TFF na ndiyo wameingia nayo mkataba katika matumizi ya Uwanja wa Taifa kwa timu za soka ingawa akataka aulizwe zaidi Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo nchini, Makoye Alex Nkenyenge.
Alipoulizwa Nkenyenge alisema: “Sijapata barua rasmi kutoka TFF inayoeleza mashabiki kuingia bure uwanjani, sisi tunafanya kazi na TFF na ndiyo inayoomba uwanja, hivyo watakapoleta barua tutajua nini cha kufanya lakini kwa sasa (‘jana jioni)’ utaratibu ni ule ule,”.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Mwesigwa Celestine hawakuwa tayari kuzungumzia utaratibu wa malipo hayo wala mgao wa TFF katika mchezo huo.
No comments:
Post a Comment