Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba, yanatarajiwa kufunguliwa leo na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ikiwa ni maonesho ya kwanza ya mpango wa pili wa miaka mitano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.
Kutokana na uzinduzi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewahimiza wananchi kufika kujifunza uanzishaji wa viwanda vidogo, kati na vikubwa.
Akizungumzia ufunguzi huo, Mwijage alisema katika maonesho hayo wenye ndoto za kuanzisha viwanda hawana budi kufika kujifunza namna ya kujenga viwanda kwa fedha kidogo wakiungwa mkono na taasisi za kifedha.
Alisema maonesho hayo yanayoshirikisha nchi zaidi ya 30 yatatumika kurasimisha biashara kwa kutumia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa muda mfupi.
“Brela itakuwepo kuonesha kuwa Tanzania ina uwezo wa kusajili kampuni kwa muda mfupi isipokuwa mtu awe na nakala muhimu,” alisisitiza.
Alisema katika kuonesha maonesho hayo yamejikita kujengea uwezo Watanzania kuanzisha viwanda vinavyozalisha bidhaa bora kuna banda maalumu lenye wataalamu wa viwanda na uwekezaji watakaotoa maelekezo ya viwanda na uwekezaji.
No comments:
Post a Comment