Na Golden Mwakatobe
Dar es Salaam. Matukio ya watu wanaokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya na nyara za Serikali yameendelea, baada ya raia wa Nigeria kunasa kwenye ulimbo wa polisi.
Kwa mujibu wa jeshi hilo, linamshikilia raia huyo kwa tuhuma za kukutwa na kilo tano za dawa za kulevya aina ya heroine zilizofichwa na kushonewa kwenye begi dogo jeusi.
Kamanda wa Polisi wa JNIA, Martine Otieno alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Bede Eke (43) aliyekamatwa uwanjani hapo juzi saa 7.25 usiku akijiandaa na safari ya kuelekea mji wa Lagos nchini Nigeria kupitia Addis Ababa kwa Shirika la Ndege la Ethiopia.
Otieno alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) walimkamata mtuhumiwa huyo kwenye mashine za ukaguzi eneo la wasafiri wanaoondoka nchini.
Alisema awali walipata taarifa za kiintelijensia kuhusi Eke na alipopekuliwa alikutwa na dawa hizo za kulevya ambazo zilifichwa kwa kushonewa kwenye begi dogo jeusi la mgongoni ambalo liliwekwa kwenye begi kubwa la nguo.
“Huyu mtuhumiwa alizificha dawa za kulevya kitaalamu ili asibainike na vyombo vya dola na alishonea pakiti kwenye begi dogo jeusi na kuliweka ndani ya begi lake la nguo, lakini tulimbaini kwenye hizi mashine za ukaguzi,” alisema kamanda huyo.
Alisema polisi inamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.
Otieno alisema polisi wataendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kudhibiti uhalifu wa aina hiyo.
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege siyo vichochoro vya kupitishia dawa hizo kwa kuwa polisi inashirikiana na wadau mbalimbali ili kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
Januari 2, mwaka huu, raia wa Nigeria, Ejiofor Ohagwu (33) alikamatwa na kilo nne za heroine uwanjani hapo.
Mei 17, mfanyabiashara maarufu wa Magomeni Makanya, Dar es Salaam Omary Kaunga (49) alikamatwa na kilo moja ya dawa za heroine na cocaine.
Katika mwendelezo wa kupambana na dawa za kulevya, jeshi hilo lilimkamata mwanamke raia wa Nigeria akiwa na kete 99 za dawa za kulevya alizokuwa amezihifadhi kwenye chupa ya mafuta ya kupaka na kopo la poda ya watoto.
No comments:
Post a Comment