Saturday, 25 June 2016

Croatia na Ureno kuvaana leo saa 4 usiku

  Na Kalonga Kasati

Michuano ya Euro mwaka 2016 inaendelea leo katika hatua ya mtoano (16 bora), ambapo kunafanyika michezo mitatu katika viwanja vitatu tofauti.
Saa kumi jioni, Poland wanacheza na Uswisi, Wales na Ireland ya Kaskazini wanachuana saa 1 usiku, wakati Croatia na Ureno wanapambana vikali saa 4 usiku.


Tukiangazia mchezo kati ya Croatia na Ureno ambao utachezwa kunako dimba la Stade Bollaert-Delelis uliopo manispaa ya Lens.

Huu ni mchezo wa kusisimua ambao unazikutanisha timu ambazo zimeamaliza hatua ya makundi na rekodi tofauti kabisa. Croatia walimaliza kama vinara wa kundi D mbele ya Uhispania, Uturuki na Jamhuri ya Czech pamoja na kumaliza ubabe wa Uhispania kutofungwa mechi 14 mfululizo katika michuano ya Ulaya, wakati Ureno walimaliza nafasi ya tatu baada ya kutoka sare michezo yote na kuingia katika hatua hii kama mshindwa bora (best loser), kwenye kundi lililokuwa na timu za Austria, Iceland na Hungary.

Kwa upande wa Croatia, leo kiungo wao mahiri Luka Modric anaweza kurejea baada ya kuukosa mchezo dhidi ya Ufaransa kutokana na majeraha ya nyonga yaliyokuwa yakimsumbua.

Kocha Ante Cacic bado hajafanya maamuzi kama amtumie mshambuliaji Mario Mandzukic au Nikola Kalinic, ambaye alifunga katika mchezo dhidi ya Uhispania.

Croatia watakuwa watakuwa na faida ya kuwa na mapumziko zaidi, lakini mshambulizi Nikola Kalinic, amekiri kwamba mchezo wa leo hautakuwa rahisi kutokana na uimara wa wapinzani wao.

“Pengine tungeweza kupata wapinzani rahisi zaidi ya Ureno katika hatua hii, lakini inatubidi kucheza kwa juhudi kama tulivyofanya kwenye hatua ya makundi, tuna nafasi kubwa ya kusonga mbele. Sisi ni moja ya timu bora katika michunao hii, na kwa uwezo mkubwa wa safu yetu ya kiungo, basi tuna nafasi kubwa ya kuibiuka na ushindi,” Kalinic amesema.

“Hii ni fursa adhimu kwa kizazi chetu katika historia ya taifa letu, na tutakumbukwa tu endapo tutafanya jambo kubwa hapa,” mshambuliaji huyo wa Fiorentina ameongeza.

Kocha wa Ureno Fernando Santos amesema kwamba kikosi chake kipo kamili na wachezaji wake wote wamefanya mazoezi jana tayari kwa mchezo wa leo.

Santos anaamini kwamba magoli mawili ya Cristiano Ronaldo katika mchezo dhidi ya Hungary Cristiano Ronaldo yatamuongezea kujiamini, vile vile amesisitiza kurekebisha mapungufu kwenye safu yake ya ulinzi yaliyosababisha kuruhusu magoli mengi katika mchezo uliopita.

“Katika hatua hii hakuna tena nafasi ya kufanya makosa ya kizembe. Lazima tuwe na uwiano mzuri kuanzia safu ya ulinzi mpaka ushambulaiji kwa sababu tunapokwenda kushambullia tunaancha mapengo mengi nyuma kama ulivyoona kwenye michezo yetu ya hatua ya makundi.” amesema Santos.

Beki wa kushoto Raphael Guerreiro amepona majeraha yake ya misuli yaliyokuwa yanamsumbua ambayo yalisababisha akose mchezo dhidi ya Hungary.

Rekodi ya mechi walizokutana

Ureno wameshinda michezo yao yote mitatu iliyopita dhidi ya Croatia, wakifunga jumla ya magoli sita na kutoruhusu hata goli moja.

Katika michuano mikubwa, wamekutana mara moja tu mwaka 1996. Ureno walishinda magoli 3-0 katika mchezo wa makundi kwenye uwanja wa City Ground  uliopo Nottingham (hata hivyo Croatia walikuwa wameshafuzu kwenda robo fainali, Ureno pia walisonga mbele).

Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni katika mchezo wa kirafiki June 2013 jijini Geneva nchini Uswisi ambapo goli pekee la Cristiano Ronaldo liliwapa ushindi Ureno.

Croatia

Croatia wamepoteza mchezo mmoja kati ya 10 iliyopita katika michunao ya Ulaya (ushindi mara sita, sare mara tatu), huku mchezo wa robo fainali dhidi ya Uturuki mwaka 2008 ukihesabiwa sare kutokana na kufungwa kwa penati.

Vile vile hawajafungwa kwenye michezo yao ya mwisho 10 ya kimataifa. Ikiwa ni michezo mingi zaidi ya timu yoyote katika michuano ya Euro mwaka huu.

Katika mashindano makubwa duniani ambayo Croatia wamewahi kushinda kwenye hatua ya makundi ilikuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia, wakati waliposhinda michezo mitatu na kumaliza nafasi ya tatu. Hawajawahi kushinda mchezo wowote wa mtoano katika Michuano ya Ulaya. (kufunga mara moja, sare mara moja)

Croatia wana rekodi ya kucheza katika uwanja huu wa Stade Bollaert-Delelis. Walicheza dhidi ya Jamaica katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998 na kushinda mabao 3-1.

Ivan Perisic amefunga na kutoa pasi za magoli saba katika michuano mbalimbali (magoli manne, pasi za magoli tatu). Ni Davor Suker pekee ndiyo mwenye rekodi bora zaidi kwa taifa hili (magoli tisa, pasi ya goli 1).

Ureno

Ureno ndiyo timu ya kwanza kutoka sare mechi zote tatu katika hatua ya makundi kwenye michuano ya Ulaya (Uefa Euro)

Ureno wamecheza michezo mingi zaidi (31) katika historia ya Michuano ya Ulaya bila kushinda ubingwa.

Hawajafungwa kwenye mechi zao 10 za mwisho za ushindani, wakishinda mara saba. Katika mechi zao zote saba walizoshinda katika mfululizo huo, kumekuwa na tofauti ya goli moja-moja tu.

Magoli yao saba ya mwisho katika Michuano ya Ulaya yamefungwa na ama Cristiano Ronaldo (matatu) au Nani (mawili).

Bado goli moja tu Ronaldo atakuwa amefikia rekodi ya ufungaji ya Michel Platini mwenye magoli nane katika michuano hii. Magoli ya Ronaldo yametokana na michuano minne wakati Platini alifunga katika mwaka mmoja tu (1984).

Ronaldo amepiga faulo arobaini katika michuano mbalimbali ya kimataifa lakini bado hajafunga hata goli moja.

Magoli yote matatu ya Ureno katika mchezo dhidi ya Hungary yalifingwa nje ya eneo la penati. Mara ya mwisho kutokea hivi ilikuwa ni mwaka 1980.

No comments:

Post a Comment