Wednesday, 29 June 2016

Padri apiga marufuku maharusi kupaka ‘Lipstick’

 

 Na Mwandishi Wetu

Waumini wanawake wanaokwenda kufunga ndoa katika  Kanisa Katoliki Parokia ya Hananasif Kinondoni, jijini Dar es Salaam wamepigwa marufuku kupaka rangi ya mdomo  ‘Lipstick’ wakati wa ibada ya misa takatifu ya ndoa.
Rangi hiyo ya mdomo ni moja ya vipodozi ambavyo hutumiwa na wanawake kwa ajili ya urembo kwa lengo la kunogesha mwonekano wake na kuvutia mbele za watu.
Uamuzi huo ulitangazwa  na Paroko wa Parokia ya Hananasif Kinondoni jijini Dar es Salaam, Padri Gasper Mtengeti, wakati wa ibada ya misa ya kumwombea marehemu Rose Michael,  iliyofanyika kanisani hapo.

Kutokana na hali hiyo Pandri Mtengeti, aliwataka wanawake kuacha kupaka rangi wakati wa misa takatifu  ambapo alitoa sababu tatu zinazotokana na Liturijia ya Ekaristi Takatifu (utaratibu wa uendeshaji wa ibada) chini ya Kanisa Katoliki.

Pandri Mtengeti alieleza sababu hizo kuwakataza maharusi wa kike kujipaka rangi ya mdomo,  ambapo alisema rangi hiyo inayopakwa huwa inasalia katika chombo kinachobeba  divai ambayo kiimani kwa dhehebu hilo ni  Damu ya Yesu Kristu.

“Siku ya ibada ya misa ya ndoa takatifu ni lazima wanandoa watapokea mwili na damu ya bwana Yesu, sasa kwa upande wa bibi harusi, rangi wanazopaka husalia katika kikombe cha hostia.

“Sababu ya pili ni kwamba, rangi ya mdomo huwa inachanganyika na damu ya Yesu wakati wanapokunywa, kitendo ambacho si chema mbele za Mungu.

“….na sababu ya tatu rangi hizo hubaki kwenye kitambaa cheupe kinachotumika kufuta kikombe cha hostia baada ya kuguswa na midomo ya mtu mara baada ya kunywa,” alisema Padri Mtengeti.

Kutokana na hali hiyo alisema ni vema kwa waumini wa kanisa hilo wakaheshimu Liturijia na maadhimisho ya misa takatifu  na kwa wale wanaotaka kupaka rangi ya mdomo siku ya ndoa  kama moja ya mapambo wanaweza wakapaka  baada ya kumaliza ibada ya misa takatifu.

Askofu Nzigilwa.
Akizungumzia katazo hilo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, alisema sheria ya Kanisa Katoliki haikatazi mabibi harusi kujipamba, bali inawezekana paroko huyo aliangalia hali ya mazingira.

Alisema kwa utaratibu katika misa takatifu ya ndoa, waumini wanaufunga ndoa wote wanapokea mwili na damu ya Yesu, ambapo kwa upande wa damu kikombe wanachonywea ni kimoja.

“Hakuna sheria ya kanisa inayokataza maharusi kupaka rangi ya mdomo lakini kuna wakati Paroko wa Parokia yoyote anaweza akaweka sheria au utaratibu wa kufuata kulingana na mazingira.

“Kwa upande wa Dar es Salaam ni kawaida kuona zinafungwa ndoa zaidi ya moja katika misa moja na wakati wa kupokea kikombe kinachotumika ni hicho hicho hivyo inawezekana Paroko aliangalia hali ya mazingira na hiyo inaruhusiwa,” alisema Askofu Nzigilwa.

Historia 
Inaelezwa kuwa kabla ya Karne ya 19, Kanisa Katoliki liliwahi kuzuia matumizi ya ‘lipstick’ kwa waumini wake kutokana na kuamini kuwa desturi ya upakaji wa rangi hasa nyekundu katika midomo ya mwanamke ilikuwa na chimbuko lake kutoka katika ibada za kishetani.

Mwanasayansi na mtafiti wa mabadiliko ya tabia za wanadamu na maisha ya wanyama Mwingereza, Desmond Morris katika kitabu chake cha “The Naked Ape (1967)” naye anaunga mkono dhana na madai hayo.

Kauli za madaktari
Pamoja na kipodozi hicho kupendwa na wanawake wengi baadhi ya rangi za midomo inaeleezwa kuwa huleta madhara kwa afya za binadamu ambapo Daktari wa Magonjwa ya Ngozi wa Hospitali ya Mwananyamala,  Dk. Hadija Shebe alithibitisha hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana Dk. Hadija,  alisema kumekuwa na madhara mbalimbali yanayotokana na rangi za mdomo ambayo mengine yanatokana na kemikali zinazotumika kutengenezea na mengine ni kutokana mwitiko wa aleji ‘Allergic reaction’.

“Endapo rangi ya mdomo haiendani na mtu huleta reaction (madhara) ambapo ndipo kuna baadhi hupasuka au kuvimba midomo na mara nyingine kuvimba mwili mzima,”alisema Dk. Hadija.

Alisema madhara yanayotokana na kemikali zinazotumika kutengenezea, mtumiaji anaweza kupata athari kwenye ngozi, figo na hata pia huweza kusababisha mtu kuugua saratani.

“Kuna baadhi ya lipstick ambazo hutengenezwa kwa kutumia madini ya risasi  na kemikali nyingine ambazo ni Aluminium, Cadium, Chromium ambazo tafiti zilizowahi kufanyika zinaonesha huleta madhara ambayo hatimaye husababisha saratani,” alisema Dk. Hadija.

Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa huko Marekani  Oktoba 2007 na  taasisi ya US Consumer Group “Campain for Safe Cosmetics” katika ripoti  iliyopewa jina la “A Poison Kiss, the Problem of Lead in Lipstick”  (Busu lenye sumu) ilionyesha kuwa lipstick nyingi karibu theluthi moja, zilikuwa na madini ya ‘lead’ kwa kiwango kikubwa zaidi ya kile kilicho salama kwa afya ya binadamu.

Ilielezwa kuwa viambato vingine vyenye madhara ambavyo vinapatikana katika rangi za  pamoja na Butylated Hydroxyanisole (BHA), Coal tar (petroleum) na aluminum (Lakes color).

Lakini pia ndani ya rangi za kupaka midomoni kuna rangi ya Carmine au natural red 4, rangi inayotokana na wadudu wekundu waliokaushwa na kusagwa kama vile ‘Red Beetles’.

Pamoja na rangi hii, baadhi ya vipodozi hivi pia huongezewa mafuta ya nguruwe au mafuta ya ubongo wa ng’ombe kama malighafi za kutengenezea vipodozi hivi ili viweze kulainisha midomo.

Watengenezaji wengine huongeza rangi za magamba ya samaki pamoja na mazao ya mimea kama vile red beets na bizari.

Wanasayansi wanaongeza kusema kuwa viambato vyenye madhara katika rangi za kupaka midomoni vinaweza kuingia mwilini au kumezwa na kusababisha athari za kiafya kama vile saratani (kansa), figo, shinikizo la damu, uchovu wa mwili usiokuwa na sababu pamoja na  kukosekana kwa usawaziko wa kihisia (mood swing).

Matatizo mengi ya kiafya yanayosababishwa na rangi hizi, hayatokei kwa haraka na ni mara chache sana waathirika wa rangi hizi kuhusisha utokeaji wa magonjwa wanayopata na mtindo wao wa maisha wa kutumia vipodozi hivi.

Kwa mujibu wa tafiti hizo inaelezwa kuwa sumu ya ‘lead’ inayopatikana katika baadhi ya vipodozi hivyo hupita katika kondo la nyuma na kufika katika ubongo wa mtoto mchanga wa mtoto alioko tumboni na kuathiri maendeleo ya ubongo na akili za mtoto.

No comments:

Post a Comment