Kutokana na kukamilika huko, utaanza utekelezaji wake rasmi wa jiji hilo kupangwa kisasa Agosti hiyohiyo.
Mahenge alisema mpango huo uliopo katika rasimu ya mwisho ya Mpango Kabambe wa Jiji la Arusha umewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo madiwani.
Hatua hiyo ni njia ya kuwezesha kupitisha kwenye vikao vya Baraza la Madiwani na hatimaye kupitiwa na Mkurugenzi wa Miji Wizarani kwa ajili ya kuanza kujengwa mji wa kisasa jijini Arusha na katika viunga vyake.
Mahenge aliyasema hayo, jijini hapa alipozungumza na wadau wa maendeleo waliokutana kwa pamoja kwa ajili ya kuchangia mada na kuona jinsi Mji wa Arusha utakavyokuwa wa kisasa.
Alisema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itapitia mpango huo mara baada ya madiwani kupitisha kwenye vikao vyao vya mabaraza, kisha utekelezaji wake utaanza rasmi Agosti mwaka huu.
“Mpango huu ni Mpango Kabambe utakaobadilisha taswira ya Jiji la Arusha na halmashauri zake hivyo ni vyema wadau wa maendeleo wakapitia mpango huu na kujadili kwa kina ili kuona Arusha,” alisema Mahenge.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega akifungua mkutano huo aliwasihi kuhakikisha wanajadili kwa kina jinsi ya kupanga mji, pamoja na kutoa mawazo yao pale wanapoona kuna mahali pa kurekebishwa kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Madiwani ili kupitishwa na kuanza rasmi.
Alisema eneo lililoandaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ni kilometa za mraba 608; Halmashauri ya Jiji la Arusha zipo kilometa za mraba 272 na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Meru zitahusika kilometa za mraba 187.
Alisema zaidi ya Sh bilioni nane zimetumika kuhakikisha majiji mawili ya Arusha na Mwanza yanapangwa vizuri hasa kutokana miji hiyo kukua kwa kasi.
Mwaka juzi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisaini mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Subrana International Pty Ltd ya nchini Singapore, kwa ajili ya kuendeleza majiji mawili ya Arusha na Mwanza na unatakiwa kukamilika Julai mwaka huu.
No comments:
Post a Comment