Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kwamba Tanzania haitapata
upungufu wa sukari kutokana na kuanza kwa uzalishaji wa sukari kwa
viwanda vya ndani.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge Suleiman Ahmed
Sadick alipotaka ufafanunuzi namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga ikiwa tatizo la upungufu wa sukari litajirudia tena.
“Tayari Viwanda vya ndani vimeanza
uzalishaji wa sukari ambapo kufikia mwisho wa mwezi Machi mwaka huu
ambao ndio mwisho wa msimu tutakuwa tumefikia lengo la uzalishaji wa
sukari kwa nchi nzima,” alifafanua Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka
wafanyabiashara kutoweka vyakula ndani ili kuviuza kwa bei ya juu
baadae, badala yake amewataka kuuza vyakula hivyo ili kuongeza
upatikanaji wa chakula nchini, kwani uongezaji wa bei wa vyakula
unaumiza wananchi wa kipato cha chini na kati.
Katika kukabiliana na tatizo la
ukame kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, Waziri Mkuu amewataka wakulima
kutumia kipindi hiki ambacho baadhi ya maeneo yanapata mvua kwa kupanda
mazao ya muda mfupi ambayo pia mazao hayo yataweza kutumika kwa msimu
ujayo.
No comments:
Post a Comment