Kamishna Msaidizi- Nishati
Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila,
(kushoto) akielezea mafanikio ya sehemu ya nishati jadidifu chini ya
Idara ya Nishati katika upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mkutano
na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema tarehe 06
Februari, 2017. Kulia ni Mtaalam wa Nishati Jadidifu, Emillian Nyanda.
Sehemu ya waandishi wa habari
wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kamishna Msaidizi- Nishati
Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila
(hayupo pichani)
Kamishna Msaidizi- Nishati
Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila,
akisisitiza jambo katika mkutano huo.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Visiwa vidogo vilivyopo katika Ziwa Viktoria vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika ifikapo Juni mwakani.
Hayo yalielezwa na Kamishna
Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi
Styden Rwebangila, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam wakati alipokuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana Sekta
ya Nishati kupitia Nishati Jadidifu chini ya Idara ya Nishati katika
upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Alisema kuwa, wakandarasi
wameshaanza kuweka miundombinu kwa ajili ya umeme wa jua ambapo
miradi hiyo inatarajiwa kukamilika kwa asilimia mia moja ifikapo mwezi
Juni mwakani.
Akielezea mipango ya Serikali
katika kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inakuwa ni ya uhakika Mhandisi
Rwebangila alisema Wizara inahamasisha vyanzo vingine vya uzalishaji wa
umeme kama vile jua, upepo, jotoardhi na kuongeza kuwa inakaribisha
wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutafiti na kutumia vyanzo
hivyo.
Alisema kwa upande wa jotoardhi
utafiti ulifanyika na kuonesha maeneo ya Songwe na Ziwa Ngozi mkoani
Mbeya na Mlima Meru mkoani Arusha yana viashiria vya jotoardhi.
Aliongeza kuwa mara baada ya
utafiti kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, visima vinatarajiwa kuanza
kuchimbwa kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jotoardhi.
Aliendelea kutaja mipango mingine
kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa mwongozo kwa ajili ya mfumo wa umeme
kwenye majengo na wa udhibiti wa matumizi ya umeme viwandani.
Alisema pia, Wizara inatarajia kuanzisha mfumo mpya wa uhifadhi data na utoaji taarifa za Nishati Jadidifu ujulikanao kama Tanzania Renewable Energy Management Information System (TREMIS) utakaowezesha wawekezaji ndani na nje ya nchi kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya Nishati Jadidifu.
Alisema katika mfumo huo
kutawekwa taarifa mbalimbali kuhusu, tafiti mbalimbali na fursa za
uwekezaji katika nishati jadidifu , sera, sheria na taratibu ili kuvutia
wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Kupitia mfumo huu kutakuwa hakuna
haja ya mwekezaji kutoka nje ya nchi kufunga safari hadi Tanzania kwa
ajili ya kupata taarifa, taarifa zote zitakuwepo katika mfumo huu
utakaounganishwa na tovuti ya Wizara,” alisema Mhandisi Rwebangila.
No comments:
Post a Comment