Kama tulivyowaeleza mwaka jana,
Shirika la Nyumba la Taifa limetekeleza ahadi yake ya kuunga mkono
uamuzi wa serikali wa kuhamia Dodoma kwa kujenga nyumba kwa ajili ya
watumishi wa serikali. Kama mnavyofahamu, kwa sasa mji wa Dodoma una
mahitaji makubwa ya nyumba kufuatia uamuzi huo wa serikali ya Awamu ya
Tano wa kuanza utekelezaji wa kuhamishia shughuli za serikali mjini
Dodoma.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
leo linazindua rasmi mradi wa kitovu cha mji wa kisasa wa nyumba za
gharama nafuu unaotekelezwa eneo la Iyumbu mjini Dodoma. Mradi huu uko
jirani kabisa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), takriban kilometa kumi
kutoka Dodoma mjini. Mradi huu ambao ujenzi wake umeanza Desemba 2016
una ukubwa wa ekari 234 na ni moja ya sehemu ya mji uliopangiliwa
kitaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni za mipango miji na utajengwa
katika awamu tatu. Ujenzi wa nyumba za awamu ya kwanza utakamilika mwezi
Machi 2016.
Awamu hii ya kwanza inahusisha
ujenzi wa jumla ya nyumba 300 za gharama nafuu. Nyumba hizi zina ukubwa
tofauti tofauti wa mita za mraba 79 zenye nyumba 45, mita za mraba 85
zenye nyumba 210 na mita za mraba 115 zenye vyumba 45. Nyumba zote hizi
zina vyumba vitatu kila moja. Ni mradi wa nyumba za chini zisizoungana,
maarufu kama stand-alone units. Mradi umesheheni huduma zote muhimu
kama vile mfumo wa maji safi na salama, umeme, maegesho ya magari, maji
ya akiba, shule ya awali, zahanati pamoja na barabara nzuri
zinazopitika.
Vilevile, Shirika la Nyumba la
Taifa limetenga, maeneo kwa ajili ya viwanja vya michezo na maeneo ya
biashara za maduka ili kuwapatia mahitaji muhimu wakazi wa Iyumbu.
Ili kuwa mmoja wa wamiliki wa
nyumba hizi Shirika la Nyumba la Taifa linakukaribisha kuanza kufanya
malipo kwa kutumia mifumo mbalimbali ikiwemo kulipia kidogo kidogo
(progressive payment plan); au kuchukua mkopo wa nyumba kutoka benki
washirika (mortage finance). Hii ni fursa ya pekee kwa Watanzania,
wafanyakazi wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali kumiliki nyumba
kwenye mradi uliopangwa vizuri wenye mandhari nzuri ya Iyumbu – Dodoma.
Nyumba za awamu hii ya kwanza ya
mradi huu zitauzwa kwa bei ya kuanzia TZS 57,670,000.00 bila kodi ya
ongezeko la thamani(VAT) mpaka TZS 83,950,000.00 bila kodi ya ongezeko
la thamani (VAT). Tunawahamasisha na kuwakaribisha Watanzania wote
kufika katika ofisi zetu za Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa
au kupitia baruapepe dg@nhctz.com ili kukamilisha mapema taratibu za manunuzi na kuwa mmoja wa wamiliki halali wa nyumba hizi.
Uzinduzi wa mauzo ya nyumba za
mradi huu ni mfululizo wa uzinduzi wa miradi ya nyumba za NHC unaolenga
kutimiza malengo ya mkakati wa Shirika wa miaka kumi 2015/16 – 2020/25.
Tunatarajia kutekeleza awamu ya pili na ya tatu ya mradi huu ambazo
zitahusisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wenye kipato cha kati na
juu pamoja majengo makubwa ya shughuli za kibiashara
Ukiwa mdau na mnunuzi mtarajiwa
unayehitaji kununua nyumba katika mradi huu, tafadhali waweza tumia
akaunti nambari 029103005062 iliyopo National Bank of Commerce(NBC) Tawi
la Dodoma au wasiliana na kitengo cha mauzo simu namba 0754 444 333;
baruapepe:sales@nhctz.com na pia tembelea tovuti ya Shirika
www.nhctz.com kwa maelezo zaidi.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO NA HUDUMA KWA JAMII
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
No comments:
Post a Comment