Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu
saba wakiwemo viongozi na wanachama wanne wa CCM ambao ni Ndg Ally
Mmbaga, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mjumbe wa Kamati ya Siasa
ya Mkoa, Ndg Arnold Swai, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya
ya Hai, Ndg Anastazia Innocent Malamsha, Mwenyekiti wa UWT Tawi la Chuo
Kikuu cha Ushirika (Moshi) na Ndg Edwin Msele, Katibu wa Hamasa wa
Shirikisho la Vyuo Vikuu Mkoa wa Kilimanjaro vilivyosababishwa na ajali
ya barabarani katika eneo la Mwika, Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoa wa
Kilimanjaro siku ya Jumapili ya tarehe 05th Februari 2017.
Ajali hiyo ilitokea majira ya
jioni ikihusisha gari ya mizigo aina ya Fuso na Toyota Hilux Surf
iliyokuwa imewabeba Viongozi wa CCM waliokuwa wakitoka katika kutekeleza
majukumu ya Chama ya Maadhimisho ya Miaka 40 ya Kuzaliwa kwa CCM
yaliyofanyika kimkoa Wilayani Rombo na kusababisha vifo vyao.
Kutokana msiba huo, Katibu Mkuu wa
CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ndugu Iddy Juma, familia, ndugu,
jamaa, marafiki pamoja na wanachama wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro kufuatia
vifo vya Viongozi wetu.
Wana CCM nchi nzima, tunawaombea
majeruhi kupona haraka, na tunamuomba Mwenyezi Mungu aziweke mahali pema
roho za Marehemu. Amina.
Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI
06/02/2017.
No comments:
Post a Comment