Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akitoa maelekezo kwa watendaji wa mkoa wa
Arusha wakati wa kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma 2016, mjini
Arusha.
Katibu
Tawala, mkoa wa Arusha Bw. Richard Kwitega akiwakaribisha watumishi wa
umma mkoani Arusha katika kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma 2016,
lengo likiwa kuwasilisha kero na maoni kuhusu Utumishi wa Umma
Mwakilishi wa chama cha wafanyakazi akiuliza swali wakati wa kikao mkoani Arusha
Mmoja wa Watumishi akiwasilisha kero kuhusu hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Watumishi waliohudhuria mkutano kazi wa Wiki ya Utumishi wa Umma 2016
mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri wa Nchi-Utumishi na Utawala Bora Mhe.
Angellah Kairuki (Mb) hayupo pichani.
Picha na mpiga picha wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki
(Mb) amewaelekeza waajiri kuhakikisha kuwa fursa za mafunzo zinakuwa
wazi na kujulikana kwa Watumishi wa Umma ili kuepuka malalamiko.
Waziri Kairuki alisema hayo wakati
wa kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2016 kilichofanyika
katika ofisi za Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha katika muda
tofauti. Kikao kilihusisha watumishi wa umma katika mikoa hiyo, ikiwa ni
pamoja na kusikiliza maoni na kero zinazowakabili.
“Fursa za mafunzo zikijulikana kwa
kila mtu zitaepusha malalamiko ya baadhi ya watu kurudia kwenda katika
mafunzo wakati wengine bado” Mhe. Kairuki alisema na kuongeza, lazima
mpango wa mafunzo kwa kila taasisi uzingatiwe ipasavyo.
Waziri Kairuki aliongeza, Maofisa
Rasilimaliwatu wanalo jukumu la kuhakikisha wanawahudumia watumishi wa
umma ipasavyo, kwa kusikiliza changamoto wanazozipata katika maeneo ya
kazi na kuzitatua kama mikataba ya huduma kwa mteja na mwongozo wa
kushughulikia malalamiko ulivyoelekeza.
Aidha, aliwaelekeza Maofisa
utumishi kuhakikisha wanamaliza zoezi la kusafisha taarifa chafu katika
Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) ili
kubaki na majina ya watumishi wanaostahili wakiwa na takwimu safi,
zisizo na shaka.
Alisema kwa wale ambao watabainika
kucheza na mfumo ili kudanganya au kuzembea hatua za kinidhamu
zitachukuliwa mara moja dhidi yao.
Waziri Kairuki aliwahakikishia
watumishi kuwa ajira zao ni salama, na wale wanaoenda kinyume na maadili
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu zilizopo.
Kuhusu vitambulisho na fomu za
wazi za mapitio na tathmini ya kazi (OPRAS) Waziri Kairuki alielekeza
kila mwajiri kuhakikisha anawahudumia watumishi na sio kuuza nyaraka
hizo. Kila mwajiri ahakikishe watumishi katika eneo lake wanapata
vitambulisho na fomu za OPRAS bila usumbufu au kuingia gharama yoyote.
Waziri Kairuki anaendelea na vikao
kazi na Watumishi wa Umma katika mkoa wa Manyara kusikiliza kero na
maoni kuhusu Utumishi, ikiwa ni moja ya matukio katika Wiki ya Utumishi
wa Umma 2016.
No comments:
Post a Comment