Wednesday, 1 June 2016

Mwezi Julai mwaka huu kuanza mfumo wa kielektroniki katika utoaji wa risiti kwa tozo, faini, ada na malipo mengine yote ya Serikali Kuu



NGO3Na Fatma Salum- MAELEZO.
Dodoma
Serikali imeagiza kuwa kuanzia Mwezi Julai mwaka huu ni lazima mfumo wa kielektroniki utumike katika utoaji wa risiti kwa tozo, faini, ada na malipo mengine yote ya Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakala wote wa Serikali ili kudhibiti upotevu wa mapato. 

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017 leo Bungeni mjini Dodoma.

Dkt. Mpango alisema kuwa agizo hilo pia linahusisha malipo ya faini za mahakamani, faini za usalama barabarani, viingilio kwenye mbuga za wanyama na vibali vya kuvuna maliasili.

“Naziagiza ofisi zote za Serikali kutoa risiti za kielektroniki kwa malipo yote yatakayofanyika kwani matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato yataongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.” Alisema Dkt. Mpango.

Katika kufanikisha hilo Dkt. Mpango aliongeza kuwa Maafisa Masuuli wote wanaelekezwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo hilo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango alisema kuwa Serikali imeamua kufanya uthamini wa majengo kwa mkupuo ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo na usimamizi wake utakuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Katika hotuba hiyo Dkt. Mpango amefafanua mkakati wa Wizara yake kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia 2016/17 hadi 2020/21 ambao umejikita katika kujenga msingi wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu.

No comments:

Post a Comment