Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mhe William Lukuvi ametoa siku 10 kwa watendaji wa
Wizara yake kumshauri ili aweze kutatua mgogoro wa makazi wa watu wa
Kinondoni Quarters.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar
es Salaam wakati Lukuvi na timu ya wataalaam wa Wizara walipokuwa
wakisikiliza malalamiko ya wakazi hao katika Wiki ya Utumishi wa Umma.
“Kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano
ni kurekebisha yaliyopinda na kutoa suluhu haraka ili kuwafuta wananchi
machozi,”alisema Lukuvi na kuongeza kuwa Serikali haitaki kuona haki za
wananchi zinacheleweshwa.
Aliongeza kuwa ni nia ya Serikali
kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapatiwa makazi bora kama ilivyo katika
ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015.
Waziri Lukuvi alisema kuhusu
makazi bora, Wizara inafanya mapitio ya Sera ya Makazi ya Mwaka 2010 ili
iweze kwenda na wakati na pia kutengeneza Sera ya Nyumba.
Awali, akitoa malalamiko,
Mwenyekiti wa Kamati wakazi waliovunjiwa nyumba zao, Bw. George Abel
alisema kuwa suala hili limechukua muda mrefu tangu mwaka 2009 hivyo
wanamuomba waziri amshauri Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt John Pombe Magufuli abatilishe umiliki wa ardhi hiyo na kuukabidhi
kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili nyumba zijengwe
na wao wako tayari kununua.
“Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni imeshindwa kujenga kwani tuliahidiwa kuwa mwaka 2011 nyumba
zitakuwa zimekamilika na sisi ndio tutakuwa wapangaji na wanunuzi wa
kwanza, lakini hadi leo ni miaka mitano nyumba hazijajengwa nasi
tunaishi kwa shida,”alisema Abel.
Aidha, Bw. Abel alisema kuwa
wakazi 644 wa Kinondoni Quarters walivunjiwa nyumba zao na Manispaa ya
Kinondoni kwa madai kuwa ni nyumba chakavu na zitajengwa nyumba za
kisasa ambazo watapangishwa na hatimaye kuuziwa jambo ambalo
halijatekelezwa hadi sasa.
No comments:
Post a Comment