Saturday, 18 February 2017

Yanga kuikabili Ngaya leo Uwanja wa Taifa

Baada ya kuifunga kwao mabao 5-1, Ngaya de MBE ya Comoro huko kwao, Yanga, wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wana nafasi kubwa leo Jumamosi kuishangaza Afrika kwa kuipiga timu hiyo ya Comoro mabao mengi zaidi hapa Tanzania.
Yanga ambayo inahitaji sare tu kesho isonge mbele katika michuano hiyo mikubwa na yenye utajiri wa pesa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, inawezekana wachezaji wa Yanga wakaingia na mawazo kuwa tayari wamefuzu kwa ushindi waliopata ugenini Jumapili iliyopita, lakini mchezo wa mpira hauko hivyo.
Yanga inapaswa kesho iingie uwanjani kama haijashinda katika mechi ya kwanza na kikubwa zaidi, Yanga inapaswa kuwania kuweka rekodi Afrika kwa kuishindilia Ngaya mabao mengi.
Mtaji huo wa mabao ndio utaipa heshima zaidi Yanga barani Afrika. Ngaya ni timu nzuri hasa katika rekodi yake ya mechi za nyumbani ambapo ilikuwa haijafungwa kabla ya rekodi hiyo kutibuliwa na Yanga ilipoifunga mabao 5-1. Yanga mna nafasi ya kujijengea umwamba barani Afrika.
Badala ya kuwaza hatua inayofuata, Yanga inapaswa kuweka akili katika mchezo wa kesho na iingie uwanjani kama iliyofungwa. Tungependa kuona timu zetu zinaweka heshima zaidi barani Afrika. Kwa sisi, tunapaswa kuweka uzalendo kwa timu zetu zinazowakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, badala ya kushangilia wageni, ni bora kukaa kimya.
Mashabiki pia tunataka soka ya kuvutia kwa timu zetu na si kuona butuabutua tu. Soka burudani yake mbali ya mabao ni mpira wa kuvutia. Yanga tupeni raha kesho na muishangaze Afrika. Binafsi naamini wachezaji wa Yanga wanaweza wakafanya makubwa kama wakiingia uwanjani huku wakiwa na kiu ya kushinda mechi, tena kwa mabao mengi.
Yanga wanatakiwa wahesabu kuwa wamecheza kipindi kimoja na kipindi cha pili watakicheza kesho, hivyo suala la kubweteka lisiwe na nafasi hata kidogo, kwani sote tunajua maajabu ya soka yalivyo. Unaweza ukajiamini kuwa tayari umeshapata uhakika wa kusonga mbele lakini wapinzani wako wakatumia vizuri hali ya kubweteka kwako na kukushambulia kisha kurudisha mabao yote.


Mpira unahitaji kujitoa kwa asilimia 100 katika kila dakika na kila mpambano, hakuna mpambano ambao unaweza kuuchukulia kuwa ni rahisi halafu ukashinda, ni lazima utaangukia pua. Basi kama ni hivyo, Yanga inatakiwa ifanye kweli mbele ya Watanzania watakaolipa viingilio vyao na kwenda uwanjani kushuhudia soka maridadi.

Kwa wale Watanzania ambao huwa wanakwenda uwanjani kwa lengo la kuwashangilia wageni, nirudie tena kuonyesha msisitizo kuwa suala hilo limepitwa na wakati na ni aibu kusikia likitendeka kwa nchi yenye raia waliostaarabika kama Tanzania.

Hivi unapata wapi nguvu ya kumshangilia mgeni? Si anakushangaa? Hivi uzalendo kwetu tutajifunza lini? Watanzania tujifunze kuunganisha nguvu. Kama tunataka kufanikiwa katika soka la kimataifa, hilo ni suala ambalo halikwepeki. Vinginevyo tutabaki kuwa watu wa Simba na Yanga mpaka siku ya mwisho ya dunia.

No comments:

Post a Comment