Na: Lilian Lundo – MAELEZO – DOdoma
Serikali imesema kwamba itafanya
uchunguzi juu ya changamoto na matatizo ambayo yamejitokeza katika mradi
wa TASAF ili kuja na mfumo mwingine bora zaidi kwa ajili ya wanufaika
wa mradi huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki
ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa
taarifa ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2016/2017
ambapo wabunge waliulalamikia mradi huo kuwa na matatizo katika maeneo
ambayo wanayasimamia.
Angellah Kairuki alisema kuwa
wizara yake itafuatilia changamato zote ambazo wabunge wamezianisha
ikiwemo utoaji wa fedha kwa kaya ambazo hazina sifa, matumizi mabaya ya
fedha za mradi kwa baadhi ya wanufaika pamoja na usimamizi mbovu wa
fedha za mradi kwa watendaji wa Halmashauri.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo
la Nzega Hussein Bashe ameishauri Serikali kutafuta mfumo mzuri wa
kuzitoa fedha hizo ili wanufaika waweze kuzitumia kwa kuanzisha biashara
ndogondoga ambazo zitawasaidia kujikimu na kuziendeleza familia zao
kiuchumi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kuwe
na utaratibu wa wanufaika kutoa mchanganuo wa namna walivyozitumia fedha
hizo ili kuleta nidhamu kwa wanufaika wanaotumia fedha hizo kinyume na
malengo yaliyowekwa.
Aidha, Mbunge wa Jimbo la
Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa katika jimbo lake kuna kaya
ambazo zimetolewa katika mradi huo kwa kukosa sifa. Kaya hizo zimeagizwa
kurejesha fedha zote ambazo walipatiwa kupitia mradhi huo, na wengi wao
hawana uwezo wa kurejesha fedha hizo.
Hivyo basi, ameiomba Serikali
kuwachukulia hatua Waratibu wa Mradi huo kwani ndio waliotoa fedha kwa
watu wasio na sifa, badala ya kuwaambia wananchi kurejesha fedha
walizopewa kwani wengi wao hawana huwezo wa kuzirejesha kutokana na
vipato vyao kwa vya chini.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati
hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Pudenciana Kikwembe amesema
kuwa, mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini umeonyesha
mafanikio makubwa, licha ya kasoro kadhaa zinazotokana na baadhi ya
Watendaji wa Halmashauri wanaohusika kukosa uwazi na uadilifu katika
uwajibikaji wao.
Hivyo basi, hali hiyo imesababisha
kubainika kwa Kaya 55, 692 zisizo na sifa stahiki lakini zilikuwa
zikinufaika na mpango hu o wa kunusuru Kaya Masikini.
Aidha Kamati imeishauri serikali
kuimarisha uwezo wa Halmashauri katika kusimamia miradi ya TASAF ili
itekelezwe kikamilifu na kwa ufanisi pamoja na kuimarisha mifumo ya
kuwatambua walengwa wa Mpango huo na kuzuia kaya zisizo na sifa
kunufaika.
No comments:
Post a Comment