Wednesday, 1 February 2017

Maadhimisho ya siku ya Ardhioevu Duniani

Capturemmm
Kesho tarehe 2 Februari, 2017 ni maadhimisho ya siku ya Ardhioevu Duniani. Siku hii inaadhimishwa duniani kote kwa kutoa elimu na kuwakumbusha watu wote kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu.
Ardhioevu ni maeneo ya ardhi yaliyopo kandokando na ndani ya Chemchem, Mito, Maziwa na mwambao wa bahari wenye kina cha maji yasiyozidi mita sita wakati wa kupwa. Ardhioevu pia hujumuisha Madimbwi, Mabwawa, Tingatinga na sehemu zote yanapokusanyika maji kipindi kirefu cha mwaka.
Tanzania hujumuika na nchi nyingine wanachama wa Mkataba wa “Ramsar” kuadhimisha siku ya ardhioevu duniani Februari 2 kila mwaka. Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ardioevu ni: “Ardhioevu Hupunguza Athari za Majanga” (Wetlands for Disaster Risk Reduction)”. Tafsiri ya kauli mbiu hii ni kwamba, Ardhioevu huzuia majanga ya mafuriko yanayoweza kutokea katika pwani za bahari, hupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza kutokana na madini hatarishi kama Zebaki, hupunguza uwezekano wa kutokea kwa baa la njaa kwa kuwa maeneo okozi wakati wa kiangazi kama vyanzo vya maji na chakula kwa binadamu na wanyama. Ardhioevu pia ni maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa chakula kama vile mpunga na mbogamboga na chanzo cha maji yanayotumika kwenye kilimo cha umwagiliaji nchini. Arhioevu pia ni sekta endeshi ya uchumi wa nchi kwa kuwa ni chanzo cha maji yanayotumika kwenye kilimo, viwandani pamoja na uzalishaji wa umeme wa maji kwa gharama ndogo.
Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya ardhi ya Tanzania ni ardhioevu ambayo ni muhimu kwa bioanwai, uchumi, shughuli za kijamii na kiikolojia. Maeneo haya ni makazi muhimu ya aina mbalimbali za viumbe hai wakiwemo samaki, viboko, mamba, ndege na viumbe wengine wasio na uti wa mgongo. Katika ikolojia ya ardhioevu tunapata bioanwai kubwa kuliko eneo lingine lolote duniani. Maeneo haya ni vyanzo vya maji kwa kipindi chote cha mwaka, huhifadhi maji na kupunguza mafuriko kwa maeneo ambayo ni hatarishi.
Maeneo haya ni muhimu kwa kuchuja kemikali zilizopo kwenye maji yaliyochafuka hususani kutoka kwenye kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani. Madini yanayochujwa kwa wingi  na ardhioevu ni pamoja na madini ya Nitrojen, Phosphorus na madini ya Aluminium na Chuma. Madini ya Nitrojen na Phosphorus husababisha kupungua kwa hewa muhimu ya oxygen kwa viumbe wa majini. Hii hutokana na kumea kwa wingi kwa mimea aina ya mwani (Algae) ambayo ikiota kwa wingi kwenye uso wa maji husababisha ukijani unaozuia mwanga wa jua kufika kwenye kina cha maji na kuzuia “photosynthesis” kutokea. Hewa ya “oxygen” itapungua majini  na viumbe maji kama samaki hufa kwa wingi.
Ardhioevu pia huzuia mmomonyoko wa udongo kwenye fukwe/kingo za mito na mifereji unaoweza kusababishwa na mawimbi ya bahari. Ardhioevu pia ni vyanzo vya umeme, na huchangia huduma ya usafirishaji na ni maeneo mazuri kwa ajili ya kubarizi.
Maeneo ya ardhioevu yanasimamiwa na mkataba wa “Ramsar” ambayo Tanzania imeweka saini, Sheria ya Usimamizi wa Wanyamapori na Mazingira yake, na ndio msingi wa usimamizi na matumizi endelevu ya ardhioevu duniani. Mkataba huu ulisainiwa na nchi wanachama kwa mara ya kwanza katika mji wa Ramsar nchini Iran mwaka 1972. Lengo la kuanzishwa kwa  mkataba huu ni kuhifadhi Ndege maji kwa mfano Korongo Taji, Korongo Nyangumi Bungunusu, Herroe Mkubwa, Heroe Mdogo. Ndege hawa ni muhimu kwa utalii na uhifadhi wa mazingira na mwingiliano wa bianuwai. Pia ni dalili ya afya ya mazingira. Tanzania iliweka saini makubaliano haya mwaka 2000.
Tanzania kuna maeneo ya Ardhioevu  manne ambayo ni; Ziwa Natron yenye umuhimu wa kuhifadhi ndege aina ya Heroe Wadogo-(Lesser flamingo), Malagarasi Muyovosi  ina umuhimu wa kuhifadhi ndegemaji aina ya  Korongo Domkiatu (Shoebill Stork), Bonde la Mto Kilombero yenye umuhimu wa uhifadhi wa Puku na Rufiji mafia Kilwa uhifadhi wa Mikoko na Mazao ya Baharini.
Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa ardhioevu nchini. Hata hivyo, ardhioevu nyingi nchini zinaharibika na zingine kutoweka kutokana na ongezeko la shughuli za kimaendeleo zisizo endelevu kama vile ujenzi kwenye vyanzo vya maji, ufugaji holela, kilimo kisichozingatia kanuni za kilimo cha kisasa na kukata miti ovyo. Athari zingine zinazotokana na matumizi mabaya ya ardhioevu ni pamoja na vifo vya mimea maji na wanyama wanaotegemea maji kuishi na kunywa kutokana na matumizi yasiyoendelevu, ukosefu wa mapato kwa jamii kutokana na kuathiriwa kwa sekta za uvuvi, utalii, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji. Binadamu, mimea na wanyama wakiwemo samaki pia huathirika kwa kukosa maji.
 
Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania inawakumbusha wananchi kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo binadamu wanatumia kila siku. Mimea na Wanyama pia hutegemea maji kutoka kwenye ardhioevu. Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhioevu, kushirikiana na Serikali na Taasisi zake pamoja na Taasisi zisizo za Kiserikali katika kuyatunza maeneo haya. Mamlaka inatoa wito kwa  wananchi kutekeleza sheria mbalimbali za uhifadhi ikiwemo Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria nyingine za kisekta kama ya Maji na Uvuvi na kuwahimiza wale wote wanaoishi kwenye maeneo ya ardhioevu na hifadhi kuhama bila shuruti.
         Martin T. Loibooki
KAIMU MKURUGENZI MKUU-TAWA
1 Februari 2017

No comments:

Post a Comment