Sunday, 5 February 2017

CCM yatimiza miaka 40 ya kuzaliwa kwake

 Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama tawala nchini Tanzania, leo Februari 5, mwaka 2017 kinaadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa kwake, ambapo Mwenyekiti wake Dkt. John Magufuli amesisitiza umoja ndani ya chama hicho.
Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamefanyika kwa mtindo tofauti, ambapo badala ya kufanyika kwa mkutano mkubwa wa chama na sherehe kama ilivyozoeleka, wanachama wa chama hicho wameshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali waliyoko, pamoja na kutembelea wagonjwa hospitalini.
Taarifa iliyotolewa jana na chama hicho, ilieleza kuwa kwa mwaka huu chama hicho kinataka kuwathibitishia watanzania kuwa ni cha wachapakazi na pia kipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.


"Hakutakuwa na mikutano ya hadhara wala sherehe za maadhimisho kama ilivyo desturi. Tutafanya shughuli za kijamii na mikutano ya ndani. Msingi wa mijadala hii ni kuandaa MWONGOZO wa CCM mwaka 2017 ambao utakuwa na tafakuri za wanachama juu ya aina ya Chama wanachokitaka.

 Kwa kuwa MSINGI wa kuundwa kwa CCM ni kuwasemea na kuwatumikia watu, tunatoa wito kwa wanachama kuadhimisha kwa kufanya shughuli za kijamii". Ilisema sehemu ya taarifa hiyo
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama hicho taifa ambaye pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza wanachama wote wa CCM, ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kuwa na umoja kwa ajili ya maendeleo ya watanzania.


"Nawapongeza wanachama wa CCM wote na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi katika kutimiza miaka 40 ya CCM. Tuendelee kushikamana, kukijenga chama kwa kuisimamia Serikali katika kuleta maendeleo kwa Watanzania" Amesema Rais Magufuli

No comments:

Post a Comment