Wananchi wametakiwa kutoa taarifa wanapoona upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya si wa kuridhisha.
Wameshauriwa kutoa taarifa kwa Bohari ya Dawa (MSD) kupitia namba za simu zilizopo katika kila kituo cha afya; kwa kamati ya afya; na kumbana mtendaji wa kituo cha afya atoe maelezo ni kwa nini hawapati dawa ilihali ubaoni zipo.
Sako Mwakalobo, kaimu mkurugenzi wa fedha na mipango wa MSD amesema hayo leo Jumanne Desemba 5,2017 wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa kati uliopitiwa upya ambao utakamilika ifikapo 2020.
Amesema kila MSD inapopeleka dawa huzikabidhiwa kwa kamati ya afya ambayo kwa angalizo walilopewa na Wizara ya Afya wanapaswa kubandika kwenye mbao za matangazo aina za dawa zilizopo.
Mwakalobo amesema Wizara ya Afya imeweka mifumo rahisi ya kutoa taarifa ya ukosefu wa dawa na kuna nafasi ya malalamiko kupelekwa kwa mganga wa eneo husika au kupiga simu moja kwa moja kwa mfamasia mkuu wa Serikali.
Amesema MSD imeweka mifumo ya kupokea malalamiko kwa njia ya simu na kuelimisha jamii kuhusu haki ya kupata dawa.
Mwakalobo amesema ununuzi na usambazaji wa dawa unafanyika kwa asilimia 80 na hadi kufikia Machi mwakani huduma itafikia asilimia 100.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya ameitaka MSD kuongeza kasi ili kwendana na wakati uliopo.
Amesema kasi ya utendaji iendane na matumizi mazuri ya fedha ili ifikie kipindi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) asipate dosari katika matumizi ya fedha za umma.
Dk Ulisubisya amesaini mkataba wa utendaji kazi kwa mkakati wa miaka mitatu na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu.
No comments:
Post a Comment