Kuwalipa walimu bahshishi kumewanufaisha wanafunzi zaidi ya 48,000 katika kujifunza stadi za Kiswahili na Hisabati
14 Decemba 2017, Dar es
Salaam: Baada ya miaka miwili ya majaribio, Twaweza, kwa kushirikiana na
Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na shirika la
Innovations for Poverty Action (IPA), wamedhihirisha kuwa kuwalipa
walimu fedha baada ya matokeo ya kujifunza kunaweza kuboresha matokeo ya
kujifunza.
Matokeo haya yamethibitisha kwamba wanafunzi wameweza kujifunza na kupata stadi stahiki kwa muda
wa mwaka mmoja kile ambacho wangeweza kujifunza kwa mwaka na nusu muhula.
Matokeo ya utafiti unaojulikana kama KiuFunza, utafiti mkubwa wa
aina yake Afrika Mashariki, yaliwasilishwa katika majadiliano na wadau
wa elimu jijini Dar es Salaam.
Kwa kipindi cha miaka miwili ya KiuFunza, Twaweza na IPA
wamefanya majaribio yafuatayo katika shule 200 kwenye wilaya 21 za
Tanzania:
- Kutoa bahshishi kwa kujifunza stadi mahususi zilizoainishwa kwa darasa kwenye kundi moja la shule (Stadi).
- Kutoa bahshishi kwa ongezeko la kujifunza kwenye kundi lingine la shule (Mashindano).
Njia zote mbili zilijaribiwa ili kulinganisha matokeo
yaliyopatikana na kundi la shule za ulinganisho ambazo walimu wake
hawakupewa bahshishi. Japokuwa mfumo wa Mashindano ni mgumu zaidi
kueleweka kuliko mfumo wa Stadi, mfumo huu huleta usawa zaidi kwa
walimu, kwakuwa wanafunzi hushindana na wenzao walio kwenye makundi
yenye uwezo unaofanana. Stadi hueleweka kwa urahisi zaidi lakini pia
huwapendelea walimu wanaofundisha wanafunzi wenye uwezo mkubwa (mara
nyingi wa shule za mijini).
Wastani wa bahshishi
waliyolipwa walimu wa masomo ni shilingi 266,315.00 sawa na karibu
asilimia 42 ya wastani wa mshahara wa kila mwezi (kabla ya kodi) mwaka
2016. Kiwango cha chini cha fedha kilicholipwa kwa walimu ni shilingi
8,100 wakati ambapo ni walimu wachache tu hawakuambulia kitu. Mwalimu
aliyelipwa kiasi kikubwa kuliko wote alipata shilingi milioni 3.6.
Mbali na kuboresha matokeo ya kujifunza, mfumo wa kuwalipa walimu bahshishi umeonekana kuungwa mkono na walimu wengi:- Walimu tisa kati ya kumi kwenye shule za majaribio wanaunga mkono wazo la malipo kwa matokeo.
- Walipoulizwa kuhusu utaratibu huu kuwa wa kisera, asilimia 63 ya walimu waliafiki kwamba Serikali iweke mfumo rasmi wa motisha kwa walimu kutokana na matokeo mazuri wakati yatakapofanyika maboresho ya mishahara (lakini asilimia 37 walisema kiwango cha malipo hayo kiongezwe na kiwe sawa kwa wote)
Mwaka 2016
- Shule 135 kutoka wilaya 21 zilizoshiriki kwenye utafiti na shule 60 zilitumika kwa ajili ya ulinganisho.
- Jumla ya wanafunzi 65,643 walifanya mtihani maalumu wakiwemo wanafunzi wa shule za ulinganisho.
- Kwa ujumla, wanafunzi 48,042 walikuwa katika shule ambako motisha ilitolewa na hivyo walifanikiwa kujifunza zaidi kuliko wenzao.
Matokeo haya ni kutoka awamu ya pili ya KiuFunza 2015 -2016.
Katika awamu ya kwanza ya KiuFunza 2013 – 2014 Twaweza ilifanya jaribio
la kupeleka fedha za ruzuku moja kwa moja shuleni (utaratibu huu sasa
unatumiwa na Serikali kuanzia Januari mwaka 2016) na Malipo kwa walimu
kwa matokeo ya kujifunza pekee na kwa kuchanganya ruzuku na bahshishi.
Awamu hii ya kwanza ya KiuFunza ilionesha matokeo chanya ya kujifunza
pale ambapo motisha kwa walimu na shule kupelekewa fedha za ruzuku moja
kwa moja vilipochanganywa. Awamu ya pili ya KiuFunza ilijaribu mifumo
makini zaidi ya utoaji wa motisha baada ya Serikali kupeleka Ruzuku ya
Uendeshaji wa Shule moja kwa moja shuleni 2016.
Twaweza imechagua kujikita kwenye kuwalipa walimu fedha za
motisha awamu ya kwanza na ya pili ya KiuFunza kwa sababu ushahidi
kutoka maeneo mbalimbali duniani unaonesha kuwa motisha huwahamasisha
walimu kuongeza jitihada katika kufundisha na kuleta matokeo chanya ya
kujifunza. Kwa kuongezea, KiuFunza (na tafiti nyingine) zinaonesha wazi
kuwa motisha kwa mwalimu na uwajibikaji ni mambo ambayo yamekosekana
shuleni. Wakati wa ziara za kushtukiza katika shule za msingi mwaka
2016:- 41% ya walimu walikuwa darasani wakifundisha.
- 27% hawakuwepo shuleni.
- 32% walikuwepo shuleni lakini hawakuwa darasani kufundisha.
- kutokana na walimu kutohudhuria darasani inakadiriwa kuwa Shillingi bilioni 793 hupotea kila mwaka, yaani hulipwa kama mishahara kwa walimu amba hawakufundisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze, anasema, “Twaweza,
kwa kushirikiana na IPA tumeonesha kuwa utoaji wa motisha kwa mwalimu
unaweza kuboresha matokeo ya kujifunza. Japokuwa kujifunza kunachangiwa
na mambo mengi, tumeonesha, kupitia utafiti huu wa kisayansi, kuwa
kuchanganya motisha na uwajibikaji kunaweza kuleta matokeo mazuri ya
kujifunza kwa wanafunzi. Huu ni ushahidi thabiti wa kile kinachoweza
kufanyika na kuwa na uhakika kuwa tukifanya hivyo watoto wetu
watajifunza.
—- Mwisho —-
Kwa taarifa zaidi wasiliana na: Annastazia Rugaba | e:arugaba@twaweza.org| t: (+255) (0) 687 222 197
Ujumbe kwa wahariri- Twaweza inafanya kazi kwa lengo la kuwezesha watoto kujifunza, wananchi kuwa na utayari wa kuleta mabadiliko na serikali kuwa wazi zaidi na sikivu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Tuna programu, wafanyakazi na ofisi katika nchi zote tatu, na utaratibu unaoheshimika kimataifa wa kujifunza, ufuatiliaji na tathmini. Programu zetu muhimu ni pamoja na Uwezo, tathmini kubwa ya kila mwaka ya wananchi barani Afrika inayopima viwango vya watoto vya kujifunza kwenye maelfu ya kaya, na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi. Pia tunashiriki kwenye masuala ya umma na sera, kupitia ubia wetu na vyombo vya habari, juhudi za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya uongozi kama vile mpango wa Ushirikiano na Serikali wazi (OGP).
- Kupata makadirio ya upotevu wa pesa za walipa kodi zinazotokana na walimu kutohudhuria darasani: walimu wa madarasa ya I, II na III kwa wastani hulipwa shilingi milioni 9 kwa mwaka (kutokana na fidia kabla ya makato ya kodi, kama walivyosema walimu). Kwa kutumia kigezo kuwa asilimia 46 hawakuwepo madarasani, walipa kodi wamepoteza shilingi milioni 4.1 kwa mwaka kwa kila mwalimu ambaye alipaswa kuwa akifundisha lakini hakuwepo darasani. Haya ni makadirio ya chini kabisa kwani gharama iliyoanishwa ni kwa walimu wa madarasa ya I, II na III, lakini ukweli ni kwamba madarasa haya na madarasa ya juu hufundishwa na walimu wakongwe ambao hulipwa mishahara mikubwa zaidi.
- Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (Basic Education Statistics – BEST) za mwaka 2016, Tanzania ilikuwa imeajiri walimu 191,604 katika shule za msingi za umma. Hii ina maana kuwa makisio ya jumla ya hasara kwa mishahara ya walimu ni shilingi bilioni 793 kila mwaka.
- KiuFunza II ilifanya majaribio ya aina mbili ya utoaji wa motisha:
- Kwenye shule ya Stadi mwalimu hupokea bahshishi kwa kila mwanafunzi kwenye darasa lake ambaye amefaulu mtihani wa stadi husika. Kwa mfano, kwenye kusoma Kiswahili, mwanafunzi wa darasa la I ambaye anaweza kusoma silabi humpatia mwalimu wake bahshishi ndogo; kama mwanafunzi anaweza pia kusoma maneno, mwalimu hupata bahshishi zaidi; kama anaweza kusoma aya mwalimu hujipatia bahshishi zaidi, na kuendelea. Na hivyo hivyo kwenye hisabati, ambapo huhusisha stadi za kuhesabu, kutambua namba, kusema namba ipi ni kubwa, kujumlisha, kutoa na kuzidisha na (kwa darasa la II na III) kugawanya.
- Kwenye shule ya Mashindano, wanafunzi walipangwa kwenye moja kati ya makundi 10 kitaifa kulingana na uwezo wao kutokana na majaribio ya mwaka uliopita. Makundi haya yalipangwa kuanzia ngazi za chini (wasioweza kusoma chochote, na wasio na ufahamu kabisa wa hesabu) mpaka ngazi za juu (wanaoweza kusoma kwa mfululizo, na kufanya hesabu vizuri). Kila kundi huhusisha wanafunzi kutoka shule za KiuFunza nchi nzima. Kwa mfano, kundi linalohusisha wanafunzi wa darasa 2 wanaoweza kusoma maneno ya Kiswahili lakini hawawezi kusoma sentensi huweza kuwa na mwanafunzi kutoka Mbozi na mwanafunzi kutoka Geita. Maendeleo ya wanafunzi hawa ndani ya mwaka hulinganishwa na kuzawadiwa. Mwisho wa mwaka, wanafunzi ambao wamefaulu majaribio vizuri sana katika makundi yao hupata nafasi za juu na huwawezesha walimu wao kupata bahshishi kubwa. Jumla ya malipo kwa kila mwalimu hutegemea nafasi ya kila mwanafunzi wake. Walimu ambao watawezesha wanafunzi wengi kushika nafasi za juu kwenye makundi yao hupatabahshishi zaidi.
- Unaweza kufuatilia kazi za Twaweza
No comments:
Post a Comment