Ndugu wanahabari,
Huu ni mwendelezo wa taarifa za
kila mwezi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kuhusu mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini
ikiwa taarifa hii ni ya mwezi Novemba 2017. Aidha taarifa hii inaendelea
kutoa maelekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kudhibiti
ugonjwa huu nchini.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01
hadi 30 Novemba 2017, jumla ya wagonjwa walioripotiwa walikuwa ni 462 na
vifo 15. Jumla ya Mikoa 10 na Halmashauri 17 zimeripoti wagonjwa wa
Kipindupindu kwa mwezi Novemba. Mikoa iliyoripoti wagonjwa wa
Kipindupindu ni Dar es salaam (14 na kifo 1), Dodoma (20 bila kifo),
Tanga (5 bila kifo), Ruvuma (73 na vifo 8), Morogoro (5 bila kifo),
Rukwa (7 na kifo 1), Manyara (13 na kifo 1), Songwe (80 bila kifo),
Mbeya (119 bila kifo), Kigoma (126 na kifo1). Halmashauri zilizoripoti
wagonjwa wa Kipindupindu ni Kinondoni (8 bila kifo), Ubungo (6 na
kifo1), Mpwapwa (5 bila kifo), Chamwino (12 bila kifo) na Bahi (3 bila
kifo), Mkinga 5 bila kifo), Nyasa (73 na Vifo 8), Kilosa (5 bila kifo),
Sumbawanga Vijijini (7 na kifo1), Kiteto (13 na kifo1), Songwe Vijijini
(80 bila kifo), Mbeya Vijijini (25 bila kifo), Mbeya Mjini (26 bila
kifo), Chunya (10 bila kifo), Kyela (58 bila kifo) na Kigoma vijijini
(10 bila kifo), Uvinza (116 na kifo 1)
Ndugu Wanahabari,
Takwimu zinatuonesha bado
maambukizi mapya ni tishio kwani kuna ongezeko la idadi ya Mikoa na
Halmashauri zinazotoa taarifa za wagonjwa ikilinganishwa na mwezi
uliopita japokuwa idadi ya wagonjwa imepungua. Mwezi wa Oktoba tulikuwa
na jumla ya wagonjwa 570 ikilinganishwa na mwezi huu ambapo tuna jumla
ya wagonjwa 462. Jumla ya Mikoa 6 na Halmashauri 11 ziliripoti wagonjwa
wa Kipindupindu mwezi uliopita ukilinganisha na jumla ya Mikoa 10 na
Halmashauri 17 zilizoripoti wagonjwa mwezi huu.
Pia takwimu za kipindupindu nchini
kwa mikoa za tangu mwaka huu uanze zinaonyesha ongezeko za ugonjwa huu,
Aidha kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2017, jumla ya mikoa 17
ilitoa taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu, ikiwa na jumla wa wagonjwa
3,839 na vifo 71 (Kama jedwali linalofuata linavyoenesha). Mikoa saba
(7) haikuripoti kuwepo kwa ugonjwa huu, mikoa hii ni pamoja na Mwanza,
Shinyanga, Arusha, Lindi, Kagera, Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.
Na. | Mkoa | Januari hadi Septemba, 2017 | Octoba,2017 | Novemba,2017 | Jumla(Januari hadi Novemba,2017) | ||||
Wagonjwa | Vifo | Wagonjwa | Vifo | Wagonjwa | Vifo | Wagonjwa | Vifo | ||
1 | Mbeya | 591 | 7 | 0 | 4 | 119 | 3 | 710 | 14 |
2 | Morogoro | 308 | 11 | 7 | 0 | 5 | 0 | 320 | 11 |
3 | Dar es Salaam | 306 | 4 | 0 | 0 | 14 | 1 | 320 | 5 |
4 | Iringa | 274 | 8 | 58 | 1 | 0 | 0 | 332 | 9 |
5 | Dodoma | 216 | 3 | 14 | 1 | 20 | 0 | 250 | 4 |
6 | Kigoma | 188 | 3 | 0 | 0 | 126 | 1 | 314 | 4 |
7 | Katavi | 133 | 1 | 0 | 0 | 0 | 0 | 133 | 1 |
8 | Tanga | 117 | 2 | 6 | 1 | 5 | 0 | 128 | 3 |
9 | Mara | 110 | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 | 110 | 0 |
10 | Pwani | 83 | 1 | 0 | 0 | 0 | 0 | 83 | 1 |
11 | Manyara | 0 | 0 | 0 | 0 | 13 | 1 | 13 | 1 |
12 | Songwe | 82 | 0 | 376 | 4 | 80 | 0 | 538 | 4 |
13 | Singida | 58 | 0 | 0 | 0 | 73 | 8 | 131 | 8 |
14 | Rukwa | 46 | 1 | 0 | 0 | 7 | 1 | 53 | 2 |
15 | Ruvuma | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 |
16 | Njombe | 10 | 0 | 0 | 0 | 0 | 0 | 10 | 0 |
17 | Tabora | 7 | 1 | 0 | 0 | 0 | 0 | 7 | 1 |
Jumla | 2816 | 45 | 461 | 11 | 462 | 15 | 3739 | 71 |
Ndugu Wanahabari,
Nchi yetu inaelekea katika majira
ya mvua ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa
Kipindupindu, hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia ugonjwa huu,
kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa.
Aidha, Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri,
Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa
wa kipindupindu. Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa
mazingira, ikiwa ni pamoja na:
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi.
- Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
- Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
- Kunywa maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa.
- Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu.
- Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
- Kutoa huduma ya kwanza katika ngazi ya jamii kwa mgonjwa yeyote mwenye dalili za kipindupindu kwa kumpatia ORS.
- Endapo ORS itakuwa haipatikani hasa nyumbani, unaweza kutumia maji yaliyochanganywa na chumvi na sukari. Maji haya huweza kuandaliwa kwa kuchanganya maji safi yaliyochemshwa kiasi cha lita moja na vijiko viwili vya sukari na nusu kijiko ya chumvi.
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
Ndugu Wanahabari,
Ni dhahiri kuwa ushirikishwaji wa
sekta zote kwa ngazi zote hadi katika jamii ni muhimu sana katika
kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara inasisitiza kuwa wadau
wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali ili
kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye halmashauri na
mikoa. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia
wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Ndugu Wanahabari,
Changamoto moja wapo katika
kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu ni upatikanaji wa maji safi na salama.
Wizara inaendelea kusisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye Halmashauri na
Mikoa yote nchini.
- Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
- Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
- Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.
- Utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, za ugonjwa wa Kipindupindu kwa kufuata miongozo iliyopo.
- Kuongeza uwajibikaji wa viongozi na watendaji (Leadership and accountability): Usimamizi wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu ni muhimu kwa viongozi na wanaowasimawa. Hii ni pamoja na;
- Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
- Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
- Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
- Kuihusisha jamii katika ngazi za chini kabisa (serikali ya kijiji/mtaa) kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu katika maeneo yao kwa kusimamiana wenyewe katiaka makundi madogo madogo yenye kaya 10 hadi 20 kufanikisha utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu wa afya. Maelekezo hayo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa kaya ambazo hazitibu maji ya kunywa, hazijajenga na hazitumii choo, wanajamii wanaochafua vyanzo vya maji na kaya au wanajamii ambao bado wanaendesha kwa siri biashara za vinywaji au chakuka zilizosimamishwa.
Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Makamu wa Raisi
alizindua awamu ya pili ya kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira yenye
kaulimbiu, “Usichukulie Poa Nyumba ni Choo”. Napenda kuchukua nafasi hii
kuhimiza ujenzi wa vyoo bora kwa kila kaya ili kuweka safi mazingira
yetu hasa ikizingatiwa kuwa ni asilimia 40 tu ya kaya hapa nchini zina
vyoo bora.
Aidha, Wizara yangu imekuwa karibu na Mikoa na Halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kufanya yafuatayo:
- Kutuma timu za wataalamu kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika kushirikiana na Mikoa na Halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu
- Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa pamoja na kupima usikivu wa dawa inayofaa kutibu wagonjwa katika mlipuko huu
- Kupeleka Vifaa tiba na dawa katika Mikoa na Halmashauri zilizoathirika kupitia kanda ya bohari ya Dawa (MSD)
- Kusambaza dawa ya kutibu maji majumbani katika Mikoa na Halmashauri zilizoathirika
HITIMISHO
Ninatambua kuwa zimekuwepo
jitihada mbalimbali, na ninawashukuru na kuwapongeza wote wanaoendelea
kupambana na ugonjwa huu. Aidha, ninaendelea kuwashukuru wataalam wa
sekta husika, mashirika ya kimataifa, watumishi, mikoa, halmashauri
pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea
kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.
Asanteni sana
No comments:
Post a Comment