Thursday, 7 December 2017

Majaliwa kuhamia Dodoma 2018


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli atahamia Dodoma wakati wowote mwaka 2018 na si 2020 kama ilivyotangazwa awali.
Amesema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atahamia Dodoma mwishoni mwa mwaka huu kwa kuwa maandalizi yapo tayari.
Waziri mkuu amesema hayo leo Alhamisi  Desemba 7,2017 wakati wa uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Dodoma.
Amesema hadi sasa watumishi 2,346 kutoka wizara zote wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia Dodoma.

Majaliwa jana Jumatano Desemba 6,2017 alikagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais eneo la Kilimani mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya mkuu wa mkoa.

Rais John Magufuli alitangaza kuhamia mjini Dodoma  katika sikukuu za mashujaa zilizofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 2016 tangu nchi ipate uhuru.

Uamuzi huo ulipokewa na Waziri Mkuu Majaliwa aliyetangaza ratiba ya uhamiaji wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano baada ya yeye mwenyewe kuhamia Septemba Mosi, 2016.
Kwa mujibu wa Majaliwa, ratiba ya Serikali kuhamia Dodoma ilianza Septemba 2016 hadi 2020 wakati nchi itakapofanya uchaguzi mkuu.
Awamu ya kwanza iliyomhusisha yeye mwenyewe, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na angalau idara moja au mbili ilianza Septemba hadi Februari 2017.
Awamu ya pili ilikuwa kati ya Machi 2017 hadi Agosti 2017 ambayo iliwahusisha watendaji wa wizara mbalimbali. Awamu ya tatu ilianza Septemba 2017 hadi Februari 2018 na ya nne Machi 2018 na Agosti 2018.

Majaliwa alisema awamu ya tano ambayo ni Septemba 2018 hadi Februari 2020 itakuwa kuhamisha watumishi wa wizara waliobakia jijini Dar es Salaam na ya sita itakuwa ni kati ya Machi 2020 hadi Juni 2020 ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais, Makamu wa Rais watahamia Dodoma.

No comments:

Post a Comment