Sunday, 24 December 2017

Viongozi wa dini watoa tahadhari kwa ukiukwaji wa haki za binadamu

Wakati Watanzania wakijiandaa kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, viongozi wa dini wameeleza mambo manne yanayopaswa kuchukuliwa tahadhari na jamii mwaka 2018.
Wameyataja mambo hayo kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, uhalifu, ubaguzi; na uvunjifu wa amani wakibainisha kuwa yalichukua nafasi kubwa mwaka huu.
Viongozi hao wametaka yadhibitiwe ili yasijitokeze tena mwakani. Kwa waumini wa Kikristo, huenda huo ukawa ndio ujumbe utakaotolewa kwa waumini katika ibada hizo za sikukuu za mwisho mwa mwaka.
Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba alisema matukio ya uvunjifu wa amani mwaka huu yalikuwa tishio, hivyo ni muda sahihi wa Watanzania kujifunza namna ya kulinda tunu ya Taifa.
“Amani ndiyo kila kitu, amani ikitoweka hakuna malengo yoyote yatakayotekelezwa, kwa hiyo jamii ijitafakari katika kipindi hiki kuhakikisha amani inadumu, matukio ya wizi, utapeli yatoweke kabisa katika jamii,” alisema.
Rais wa Baraza hilo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema jamii inatakiwa kujenga utamaduni wa kulinda amani ya nchi, kutenda haki na kuhimiza upendo.
“Tunaelekea kwenye Krismasi tujali haki, tujali amani ya nchi yetu na upendo. Tumwombe Mungu atuongoze zaidi katika kipindi hiki, atusaidie katika kilimo chetu kwa sababu mvua haijaanza kunyesha,” alisema.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Rajab Katimba aliwataka Watanzania kujitathmini na kutenda haki ili mwaka ujao uwe wa amani na kila mwananchi ajisikie huru kuishi katika nchi yake.
Alibainisha kuwa, mwaka huu umekuwa na matukio mengi ambayo yanaonyesha ukiukwaji wa haki za binadamu.
Aliyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni mauaji, baadhi ya watu kufungwa bila hatia na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha. “Tumeshuhudia matukio ya kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na watu kupotea. Hivi ninavyoongea kuna mwandishi mmoja (Azory Gwanda) naye amepotea. Tunataka viongozi wahakikishe haki inatendeka katika Taifa hili,” alisisitiza.

Kiongozi huyo ametaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi ili kulinda haki za Watanzania na hasa wanyonge wasio na sauti, akisisitiza haki ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani.

“Bila haki Taifa linakufa. Uwanja wa siasa nao uwe huru ili vyama vya upinzani navyo vipate haki ya kufanya siasa kwa mujibu wa sheria na Katiba,” alisema.
Kwa mtazamo wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Jacob Chimeledya alisema sasa ni wakati wa kila Mtanzania kutambua thamani ya mtoto na kumlinda ili akue katika njia iliyo bora na baadaye kuwa msaada kwa Taifa.
Dk Chimeledya alimtaka kila mwananchi kuangalia namna atakavyogusa maisha ya mtoto kwa kila anachokifanya ili kumjengea mustakabali mwema kimaadili, kielimu na kimaendeleo.
“Maisha ya mtoto ni tunu kwa Taifa, hivyo akitunzwa ana faida kubwa baadaye. Mungu amepandikiza karama na vipawa kwa kila mtoto, kama hakutunzwa vizuri basi anapoteza karama na vipawa hivyo,” alisema.

Aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wa kutunza watoto wao katika misingi ya haki, imani na maadili ya Taifa.
Akizungumzia mwaka huu, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema umekuwa na changamoto nyingi kwa sababu wananchi hawakuzoea kuona yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwamo matumizi mazuri ya rasilimali.
Alisema ni wakati wa wananchi kujipanga kuijenga nchi iwe yenye kujitegemea, isiyoyumbishwa na mataifa mengine na kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa yao wenyewe, “Tujenge nchi yetu kwa pamoja maana nchi hii ni yetu sote. Tujenge umoja wa kitaifa, wanadini na wanasiasa tujenge utamaduni wa kuvumiliana,” alisema.
Kuhusu haki za binadamu alisema, “Watanzania hawapati maelezo ya kutosha kwa mambo kadhaa kama vile miili ya watu inayookotwa fukweni na wengine kutoweka. Hatutarajii kuendelea na hali hiyo mwaka ujao.”

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo alisema, “Ubaguzi ni mbaya watu wanapaswa kuheshimu sheria na Katiba ya nchi, tunapaswa kuishi vyema bila kujali tofauti zetu za kisiasa na kidini.” alisema.

No comments:

Post a Comment