Friday, 8 December 2017

Msigwa :Wanaohama upinzani ni waoga

  Related image
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema wanasiasa wanaohama kutoka vyama vya upinzani kwenda CCM, wanafanya uamuzi huo kutokana na uoga.
Msigwa amesema hay oleo Ijumaa wakati akihojiwa katika kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na televisheni ya Azam akiwa na Mbunge wa Temeke, (CUF) Abdallah Mtolea.

Msigwa amesema kufanya siasa ndani ya CCM kuna urahisi kuliko kufanya nje ya chama hicho kwa sababu unafanya siasa ukiwa unazungukwa na polisi na unakuwa unalindwa lakini unapokuwa upinzani unakuwa kama yatima, hali inayopelekea wengine waoga kushindwa na kuamua kwenda CCM.
“Hawa wenzetu wanaochukuliwa mi naamini kuna uoga na kuna kununuliwa, mtu akisema sisi wapinzani tuwananunua watu wa kutoka CCM, unawanunua watu wa CCM waje kufanya nini upinzani, kuna mabomu, kuna dhiki, yani mtu atoke CCM ambapo analindwa aje upinzani kwenye dhiki? Kwa hiyo hii propaganda kuwa upinzani nao unanunua watu ni ya kutaka kupotosha umma tu,” amesema Msigwa.
Msigwa ameongeza kuwa gharama za kuwa upinzani ni kubwa ndio maana hata idadi ya wanasiasa wanaohama kutoka upinzani kwenda CCM ni wengi kuliko wanaotoka CCM kwenda upinzani na ndio maana hata baadhi ya wanasiasa hao baada ya kuona hali ya joto kisiasa imezidi kuwa kali wametangaza kurudi nyumbani CCM.
Akichangia mada katika mjadala huo kuhusu wimbi la wanasiasa wanaohama vyama vya siasa Mtolea alikosoa wanasiasa wanaohama vyama na kuacha ubunge kwa kutoa sababu za kuunga mkono juhudi za Serikali.
“Hawa wanaosema kwamba wamefurahishwa na kazi ya Rais, hivi kumuunga mkono Rais ndio umtie hasara, kwa sababu ukijivua ubunge, jimbo lile unaliacha wazi na uchaguzi lazima ufanywe kwa matakwa ya sheria, leo kurudia uchaguzi kwa jimbo moja ni takriban Sh70bilioni, sasa Je unamsaidiaje Rais kwa kuitia hasara Serikali kwa kurudia uchaguzi kwa gharama hizo.”
Mtolea amesema baadhi ya wanasiasa waliotangaza kuondoka upinzani kwa kudai upinzani umeishiwa ajenda, wasichokifahamu ni kwamba vyama vya siasa haviendeshwi kwa ajenda bali vinaendeshwa kwa itikadi au misingi iliyosababisha kuundwa kwa chama cha siasa ili waweze kumaliza kero mbalimbali nchini na njia ya haraka ya kufikia maendeleo ya nchi.


Mtolea alitolea mfano tatizo la kukatika kwa umeme kuwa linaweza kuwa ajenda lakini tatizo hilo likiisha, ajenda hiyo inakua imekwisha, lakini itikadi ya chama inabaki.

No comments:

Post a Comment