Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ametoa siku 30 kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (Taa) kuziondoa familia 59 zilizo ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).
Pia, ameitaka Taa kuhakikisha hatimiliki za ardhi za kampuni ya Puma Energy na Tanzanair zinafutwa kwa sababu ziko ndani ya uwanja huo ambao nao una hatimiliki yake.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembelea kampuni hizo, Nditiye alisema haiwezekani kukawa na watu wengine wanaomiliki ardhi katikati ya uwanja huo na wana hatimiliki.
Pia, aliitaka mamlaka hiyo kuwaondoa watu wote waliojenga karibu na uzio wa uwanja huo bila kuacha mita tatu kama inavyotakiwa katika sheria ya ardhi au mita 10 kwa mujibu wa sheria ya viwanja vya ndege.
Naibu waziri huyo aliagiza viwanja vyote viwekewe mipaka na kwamba, vile ambavyo havina hatimiliki navyo vitafutiwe.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inazirudisha na kuzitambua mali zake zote. Hakikisheni viwanja vyote nchini vinakuwa na hatimiliki, mpaka sasa uwanja wa Mwanza hauna hatimiliki,” alisema. Nditiye aliitaka Taa kuhakikisha kwamba inapata taarifa zote za Puma Energy inayouza mafuta ya ndege ili waweze kukusanya tozo zao na pia kuimarisha usalama kwa usafiri wa ndege. “Wekeni watu wenu pale Puma kwa saa 24 ili mjue mafuta hayo yanatumikaje na mnapata stahiki yenu. Sasa kama mtu anaagiza mafuta na hakuna mtu anayemsimamia inakuwaje? Hiyo ni hatari hata kwa usalama,” alisisitiza.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa Taa, Richard Mayongela alisema watatekeleza maagizo yote.Hata hivyo, alishauri kwamba mamlaka hiyo ipokee tozo zao bandarini wakati mafuta yakishushwa kama ilivyo kwa mamlaka zingine za Serikali kama vile TRA.
Alisema hatua hiyo itapunguza gharama nyingine na kurahisisha ukusanyaji wa mapato wanayostahili kupata kutokana na mafuta ya ndege.
Kuhusu fidia kwa wananchi, Mayongela alisema mamlaka yake kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji wameandaa ardhi kwa ajili ya kaya zaidi ya 1,000 zilizoathirika na mradi wa upanuzi wa uwanja na tayari wamelipa Sh3.7 bilioni.
Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba timu yake imekutana na Waziri Lukuvi ambaye amewataka kupeleka nyaraka muhimu kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Kuhusu Puma Energy na Tanzanair kumiliki viwanja katikati ya uwanja wa JNIA, Mayongela alisema zilipata ardhi kihalali kwa sababu Serikali haikuwa na utaratibu wa kupima maeneo yake na mengi yalianzishwa kwa matamko.
Alisisitiza kuwa taratibu za kufuta hatimiliki zao zinaendelea ili sehemu yote ya uwanja imilikiwe na Taa.
No comments:
Post a Comment