Friday, 3 November 2017

Nyalandu azungumzia ya moyoni kuhusiana na Chadema

Lazaro Nyalandu amefunguka na kusema kuwa yeye aliviangalia vyama vya upinzani nchini na kuamua kujiunga na CHADEMA baada ya kuachana na CCM kwa kufuata ushauri wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye aliwahi kusema CHADEMA ifae.
Nyalandu amesema hayo alipokuwa akihojiwa na DW na kusema mpaka sasa bado hajajiunga na CHADEMA lakini amefikiria kujiunga nao baada ya kuvitazama vyama vingine vya siasa na kuona huko ndiko kunaweza kuwa sehemu sahihi kuwepo kwa sasa.
"Mpaka sasa bado sijafanya hatua yoyote ile ila nimeviangalia vyama vyote vya upinzani na kuangalia chama kimoja kimoja kwa sababu ilikuwa ni lazima niamue kuwa kwenye chama fulani nikakumbuka ushauri wa Baba wa Taifa alivyoitazama na yeye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere marehemu Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi, alisema CHADEMA ifae na mimi nimevitazama vyama vingine ni vizuri vinajitahidi na vipo kwenye hatua mbalimbali katika kukomaa kwao lakini kwa kweli nimeona chama ambacho mimi ningependa kuongeza nguvu ni CHADEMA" alisisitiza Nyalandu.

Lazaro Nyalandu toka alipotangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge aliondoka nchini Tanzania na kwenda nchini Kenya ambapo mpaka sasa yuko nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment