Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuandaa sheria ambayo itaondoa utaratibu wa kulipa kodi ya pango kwa miezi sita au mwaka kwa nyumba za makazi.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum Mh. Halima Bulembo aliyetaka kujua ni lini serikali itatunga sheria itakayompa nafasi mpangaji kulipa kodi ya mwezi mmoja na si miezi sita au mwaka kama ilivyosasa.
“Wizara tayari imeshaliona hilo na tupo kwenye mchakato wa kuanzisha mamlaka itakayosimamia masuala yote ya nyumba, katika sheria inayoandaliwa kwaajili ya kuletwa bungeni imeangalia ukomo wa kutoa kodi hivyo hiyo ya miezi sita haitakuwepo”, amesema Mh. Mabula.
Aidha Naibu waziri huyo ameongeza kuwa baada ya sheria hiyo kupitishwa kodi itakuwa inatolewa kwa mwezi mmoja mmoja. “Kodi itakuwa inatolewa kwa mwezi mmoja mmoja wakati huo mpangaji atalazimika kutoa amana ya miezi mitatu kwaajili ya mambo mengine yanayoweza kujitokeza”, ameongeza.
Mh. Halima Bulembo ameuliza swali hilo kwa kuzingatia malalamiko ya vijana wengi ambao ni zaidi ya asilimia 55 nchini kuwa wanashindwa kutimiza malengo yao kutokana na gharama za kulipa kodi kwenye nyumba za makazi kuwa kubwa huku wamiliki wakiomba kulipwa kwa miezi sita hadi mwaka mmoja.