Thursday, 23 November 2017

Maafisa Habari nchini watakiwa kuwa na uelewa wa Siasa na Uchumi



Mkurugenzi wa Idara ya Habari ya MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas  amesema Maafisa Habari na Mawasiliano hapa nchini wanatakiwa kuwa na uelewa wa masuala mbalimbali ikiwemo Uchumi, siasa na jamii katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Abbas ameyasema hayo leo, Mjini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya Itifaki na Mawasiliano ya Kimkakati kwa Maafisa Habari na Mawasiliano kutoka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi yaliyoandaliwa na Idara ya Habari MAELEZO kwa kushirikiana na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na  Washauri wa Kidiplomasia wa Kiuchumi (Economic Diplomacy Consultants).
 "Itifaki ni moja ya eneo ambalo Afisa Habari yoyote anatakiwa kulijua kwa undani kutokana na jukumu alilonalo la kusimamia matukio mbalimbali yanayotokea katika Taasisi yake," alisema Dkt. Abbas.
Ameendelea kwa kusema, kuna kipindi Afisa Habari anapata wageni ambao ni wakuu wa nchi na kushindwa kujua namna ya viongozi hao wanavyotakiwa kukaa kutokana na vyeo vyao.Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo mengine mengi ambayo Maafisa hao watakuwa wakiyapata kila wakati ili kuwapa uelewa katika maeneo mbalimbali ya masuala ya uchumi, siasa, jamii na katika sekta yenyewe ya mawasiliano.   
"Itafika kipindi tutajifunza hata vyeo vya jeshi namna vinavyokuwa pamoja na majina ya vyeo vyao ambapo itarahisisha katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Maafisa Habari," alisema Dkt. Abbas.
Mafunzo hayo ya Maafisa Habari na Mawasiliano  ni ya siku mbili ambayo yameanza leo Novemba 23 na yanatarajia kumalizika kesho Novemba 24, 2017.

No comments:

Post a Comment