Sunday, 26 November 2017

Tanroads yabomoa Wizara ya maji Ubungo


Kazi ya ubomoaji majengo ya Wizara ya Maji yaliyoko eneo la Ubungo mkoani Dar es Salaam imeanza
Kazi hiyo iliyoanza leo Jumatatu Novemba 27,2017 ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli ambaye aliagiza majengo ya wizara hiyo na ghorofa la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.
Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.
Katika majengo ya Wizara ya Maji, tingatinga limevunja ukuta, huku watu wengine wakiendelea na kazi ya kuondoa madirisha na milango kwenye majengo. Jengo lililoanza kubomolewa ni la ofisi ya Waziri wa Maji.
Wafanyakazi wa wizara hiyo wanaendelea kutoa mali ndani ya majengo waliyokuwa wakiyatumia kwa ofisi.
Mbali ya majengo hayo, Tanraods inaendelea kuweka alama ya X kwenye nyumba za wananchi zilizo katika hifadhi ya barabara ikiwa ni pamoja na kupisha ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo.
Tayari nyumba takriban 1,200 zikiwamo tano za ibada, vituo vya mafuta na baa katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho zimewekwa alama kwa ajili ya ubomoaji.

Kwa mujibu wa Tanroads, ubomoaji katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho unahusisha nyumba zilizo mita 91.7 katika hifadhi ya barabara ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Barabara ya mwaka 1932.

No comments:

Post a Comment