Sunday, 5 November 2017

Marekani yawaambia raia wake kuondoka Mogadishu kufuatia tishio la usalama

Jeshi la Marekani linaloendesha oparesheni dhidi ya wanajihadi nchini Somalia limewaonya raia wa taifa hilo ambao hawana shughuli muhimu kwa sasa kuondoka mjini Mogadishu mara moja kufuatia tishio la usalama katika uwanja wa ndege wa mji huo.
Onyo hilo linakuja saa kadhaa baada ya jeshi la Marekani kuthibitisha kutekeleza mashambulizi yake ya kwanza dhidi ya ngome za wanajihadi wa Islamic State katika taifa hilo la pembe ya Afrika.
Kupitia tovuti yake jeshi la Marekani limeandika kuwataka wafanyakazi wasio na ulazima ambao ni raia wa Marekani kuondoka mjini Mogadishu hadi pale watakapoarifiwa.
Marekani imefanya mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani dhidi ya wapiganaji wa kundi la Islamic State nchini Somalia, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Marekani kushambulia wanajihadi Somalia.

Mashambulizi yalitekelezwa katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Somalia na kuua "magaidi kadhaa taarifa ya jeshi la Marekani barani Afrika imeeleza.

No comments:

Post a Comment