Jukata hivi karibuni lilitangaza kufanya maandamano ya amani nchi nzima Oktoba 30,2017. Hata hivyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliyazuia ikitoa sababu tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 4,2017, Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda amesema wamefikia uamuzi huo baada ya sababu zilizotolewa na polisi kuzuia maandamano hayo kuwa nyepesi.
Mwakagenda amesema polisi katika barua ya kuzuia maandamano imeeleza kuwa, Rais John Magufuli ambaye Jukata ilimuomba kupokea maandamano hayo hajathibitisha kushiriki, kufanya maandamano umbali mrefu Mwenge hadi Mnazi Mmoja kutaathiri shughuli kwa kufunga barabara na kwamba, Oktoba 30,2017 mitihani ya kidato cha nne itakuwa ikiendelea kufanyika nchi nzima.
"Tumefikia uamuzi wa kwenda kufungua kesi mahakamani kudai haki ambayo inaminywa na kukandamizwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia sababu nyepesi,” amesema.
Amesema, “Tupo katika hatua za mwisho kutekeleza uamuzi huu na jopo la mawakili wasomi wasiopungua 10 watahusika kudai haki ya kufanya maandamano ya amani," amesema Mwakagenda.
Amesema nchi za kidemokrasia zinazofuata utawala wa sheria, mhimili wa Mahakama ndicho chombo mahsusi cha kutoa haki pale mtu au watu wanapoona haki zao zimenyimwa au zimekandamizwa.
Mwakagenda amesema Mahakama itaeleza ni kwa namna gani wananchi wanapaswa kutumia haki zao za kikatiba bila kuzuiwa, kuwekewa vikwazo au kusumbuliwa na Jeshi la Polisi.
Ameitaja sababu nyingine ya kwenda mahakamani ni kuomba tafsiri ya Mahakama kuhusu namna Jeshi la Polisi linavyotumia vifungu 43 (3) na 44 vya sheria ya jeshi hilo ya mwaka 2002.
"Kwa mtizamo wetu, Jeshi la Polisi limekuwa likitumia vibaya vifungu hivi kuzuia mikutano na maandamano ya amani kinyume cha uhalisia wa vifungu hivyo," amesema.
Amesema visingizio vimekuwa vikitolewa kwamba, kuna taarifa za kiintelijensia za viashiria vya uvunjifu wa amani.
"Tunaamini Katiba Mpya inahitajika sasa zaidi kuliko wakati mwingine kutokana na utafiti wetu na wa Twaweza uliotolewa Oktoba 19,2017 ambao ulionyesha asilimia 67 ya wananchi wanaona ni bora kupata Katiba Mpya," amesema.
No comments:
Post a Comment