Magari yakipita katika makutano ya barabara za Morogoro na bibi titi Dar es Salaam baada ya mvua iliyonyesha kwa saa mbili jana
Dar es Salaam. Mvua iliyonyesha kwa saa mbili katika maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jana, imeleta kero kwa wasafiri wa
vyombo vya moto na watembea kwa miguu na kusababisha baadhi ya barabara
kushindwa kupitika kutokana na kujaa maji.
Mvua hiyo iliyoanza saa nne asubuhi hadi saa sita
mchana, ilisababisha baadhi ya barabara kutopitika ikiwamo ile ya Samora
karibu na Jengo la Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya maeneo ya
Upanga na Msasani.
Aidha, watumiaji wa Barabara za Azikiwe, Bibi Titi
na Morogoro katikati ya jiji walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi
walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji
hayo ambayo yalionekana kuchanganyika na majitaka yaliyotokana na baadhi
ya chemba kujaa.
Eneo linalojengwa njia za mabasi ya haraka katika
eneo la Akiba, lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo
vya moto na watembea kwa miguu.
Maeneo ya Kariakoo, Barabara ya Uhuru na Msimbazi,
yalijaa maji kama ilivyokuwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuelekea
Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo zilikuwa hazipitiki kutokana na mvua
hizo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Wakazi wa mabondeni walianza kuingiwa na hofu ya
kukumbwa na mafuriko wakati hali ya hewa ilipokuwa inabadilika huku mvua
ikiongezeka kwa kasi. Katika bonde la Msimbazi, Kigogo na Jangwani
wakazi walionekana wenye hofu baada ya mvua kuongezeka.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe
alikataa kusema lolote na kusukuma mpira kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Ilala, Isaya Mgurumi.
Hata hivyo, Mgurumi alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), Agnes Kijazi alisema hayo ni matokeo ya taarifa ya hali
ya hewa waliyoitoa Oktoba, Novemba na Desemba ambayo yalibainisha kuwa
kutakuwa na vipindi virefu vya jua katika msimu wa mvua pamoja na mvua
kubwa. Alisema mvua zilizonyesha jana, zinanyesha mwisho wa msimu wa
mvua kama ilivyotabiriwa kabla.
Kijazi alisema kesho (leo) wanatarajia pia mvua
kubwa kutokana na kuwapo kwa mkandamizo mkubwa wa hewa katika pwani ya
Madagascar.
“Kesho (leo) tutatoa taarifa nyingine ya hali ya
hewa kwa kipindi cha miezi mitatu mingine, hivyo wananchi watumie
taarifa hiyo katika mipango yao mbalimbali,” alisema mkurugenzi huyo.
Wakazi walonga
unazani nini kifanyike kuondoa tatizo hili linalosababishwa na mvua ndogo tu ya masaa mawili
ReplyDeletemhhh hayoo majanga
Delete