MV Victoria
Jana katika gazeti hili tulichapisha habari iliyokuwa ikielezea
watumiaji wanaotegemea meli ya Mv Victoria, Jumatano walipata adha ya
usafiri baada ya kusitishwa kwa safari ya kuelekea Mwanza, hatua
iliyochukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(Sumatra) kwamba ilitoroshwa bila kukaguliwa.
Habari hiyo ilimkariri Ofisa Mfawidhi wa mamlaka
hiyo mkoani Kagera, Kapteni Alex Katama akisema awali, meli hiyo
ilizuiliwa Mwanza kwa ajili ya matengenezo na kwamba haikufanyiwa
ukaguzi kabla ya kuruhusiwa na akisisitiza kuwa meli hiyo bado mbovu.
Ilielezwa kuwa ilipofika Bukoba ikitumia injini
moja bila ruhusa ya mamlaka, waliizuia mpaka itakapofanyiwa ukaguzi na
kujiridhisha.
Hadi inazuiliwa, ilikuwa ikijiandaa kwa safari hiyo ya Mwanza na tayari mizigo ilikuwa imeshapakiwa.
Hata hivyo, Meneja Masoko wa Shirika la Huduma za
Meli, Obed Tirugumila alikaririwa akisema kuwa Mv Victoria ilifanyiwa
matengenezo Mwanza, lakini haikufanyiwa majaribio na maofisa wa ukaguzi
wa Sumatra akidai kuwa walisema hawana nafasi.
Hivyo, waliamua kufanya majaribio kwa kwenda Bukoba wakiwa na abiria na kufika salama.
Ni miaka 18 sasa tangu Meli ya Mv Bukoba izame
ndani ya Ziwa Victoria Mei 21, 1996 ikitokea Bandari ya Bukoba kwenda
Bandari ya Mwanza na kuua zaidi ya watu 1,000 kutokana na kuzidisha
mizigo na abiria.
MV Bukoba ilizama ikiwa imebakisha umbali mfupi
kufika Bandari ya Mwanza, lakini ukosefu wa vifaa vya uokoaji
vilisababisha kuongezeka idadi ya watu waliokufa.
Waokoaji wa ajali hiyo walisubiriwa kufika nchini
kutokea Afrika Kusini, ambao waliweza kuogelea na kuokoa baadhi ya maiti
chache zilizokuwa zimezama umbali wa mita 25 chini ya maji.
Serikali ilimshtaki aliyekuwa nahodha wa Mv
Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (sasa marehemu), Mkaguzi wa Mamlaka ya
Bandari Gilbert Mokiwa; aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce
Sambo na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 2011 ajali nyingine
mbaya ya Meli ya Spice Islander iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda
Pemba ilizama na kuua watu 240.
Tume iliyochunguza ajali ya meli hiyo ilisema meli
hiyo ilibeba zaidi ya abiria 2,000 ingawa maelezo ya nahodha wa meli
alidai kuwa melini kulikuwa na watu 500.
No comments:
Post a Comment