Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mheshimiwa Eng. Christopher Kajoro Chiza (Mb) ameeleza kuwa, kilimo cha umwagiliaji kina nafasi ya kuchangia asilimia 25 ya chakula kinachozalishwa nchini. Aliyalisema hayo wakati alipotembelea mradi wa umwagiliaji wa Nkoanrua katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru.
Azma hiyo inaweza kufikiwa kwa kuongeza eneo, pamoja na kuongeza tija katika maeneo yaliyopo. Hatua za kuchukua ni pamoja na kubadili kilimo cha kujikimu kuwa cha kibiashara.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo itafikiwa endapo wakulima watabadilika na kulima kilimo cha kisasa badala ya kilimo cha mazoea.
Hatua nyingine ni kukarabati na kuisafisha mifereji ya umwagiliaji iliyopo kwa lengo la kupunguza upotevu wa maji ili kuleta ufanisi katika matumizi ya maji. Vile vile aliwahimiza wakulima kuzalisha mara mbili katika msimu, aliongeza Mheshimiwa Chiza.
Aidha, alihimiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na kuwa na Kamati ya watumia maji ili kuboresha huduma za umwagiliaji.
Hatua hizo zitawezesha kufikiwa kwa malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambapo ifikapo mwaka 2015 kuwe na ongezeko la mavuno kwa zao la mahindi la tani 100,000, mchele tani 290,000 na Sukari tani 150,000.
No comments:
Post a Comment