Akizungumza na gazeti hili juzi mchana kwa njia ya simu kutoka Kigali, Rwanda, Niyonzima alisema atarejea nchini mara tu hali ya watoto wake itakapokuwa vizuri.
Niyonzima alisema anafahamu majukumu yake ndani ya klabu na kinachomchelewesha kurejea nchini, ni kutekeleza majukumu yake kama baba wa familia.
"Nitarudi hivi karibuni Inshaallah, hivi tunavyoongea na wewe niko hospitali, nipigie baadaye tutaongea zaidi," alisema kwa kifupi Niyonzima alipozungumza na gazeti hili juzi Julai 7, mwaka huu saa 6:19 mchana kwa saa za Tanzania sawa na saa 5:19 kwa saa za Kigali, Rwanda.
Jana kiungo huyo hakuweza kupatikana tena katika simu yake ya mkononi inayoishia na namba ...719 kuelezea zaidi tatizo linalomchelewesha kurudi nchini kushiriki kwenye mazoezi pamoja na wachezaji wenzake.
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, aliliambia gazeti hili Jumapili kwamba klabu haijafurahishwa na kitendo cha Niyonzima kuchelewa kwa muda wa mwezi mmoja wakati huu ambao wachezaji wenzake wameshaanza mazoezi.
Tiboroha alisema haiwezekani mchezaji achelewe muda huo bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.
"Haiwezekani mchezaji achelewe mazoezini mwezi mzima, atakaporipoti ni lazima ajieleze kabla ya hajachukuliwa hatua," alisema Tiboroha Jumapili iliyopita.
Katibu huyo aliongeza kwamba ni lazima suala la nidhamu liwekwe kwa wachezaji wote na si kuwapendelea nyota wa kimataifa kwa kutowaadhibu pale wanapokwenda kinyume cha taratibu.
Yanga ambayo itaanza kampeni za kuwania ubingwa wa Kombe la Kagame kwa kuwakaribisha Gor Mahia ya Kenya, ilianza mazoezi kujiandaa na michuano hiyo na msimu ujao wa Ligi ya Bara tangu Juni 8, mwaka huu ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa.
Niyonzima alirejea kwao Rwanda pamoja na familia yake tangu Mei mwaka huu baada ya ligi msimu uliopita kumalizika.
Tayari Yanga imeshacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Friends Rangers ya Magomeni jijini Dar es Salaam na jana jioni iliikaribisha KMKM ya Zanzibar katika mchezo mwingine wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa.
KMKM ambayo iko chini ya Kocha Mkuu, Ali Bushiri, pia inajiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame ambayo yanatarajiwa kushirikisha klabu 13 kutoka Afrika Mashariki na Kati.
No comments:
Post a Comment