Sunday, 5 July 2015

Mbinu hii imefeli Spika, maridhiano kwanza


Spika wa Bunge, Anne Makinda

Jana, Spika Anne Makinda alilazimika kuahirisha shughuli za Bunge asubuhi baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kupiga kelele na hivyo kusababisha muwasilishaji wa Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 asisikike vizuri.
Hii ni takriban mara ya tatu kwa shughuli za Bunge kushindikana kutokana na wabunge hao kutokubaliana na hali ya uendeshwaji wa vikao na hoja za Serikali na hivyo kuamua kuweka mazingira ambayo hayaruhusu kazi yoyote kufanyika.
Juzi, wabunge walidai kuwa miswada hiyo iliwasilishwa kwenye semina na wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, waliazimia kuwa suala hilo lifanywe na Bunge lijalo. Bunge lilipotaka kuendelea na shughuli zake ndipo kelele hizo zilipoanza na Spika kulazimika kuahirisha kikao.
Jana tena walistukia miswada hiyo ikiwasilishwa na walipotaka mwongozo, Spika hakusikiliza na hivyo kusababisha wabunge wa upinzani kusimama na kuanza zogo lililosababisha kiongozi huyo wa Bunge ashindwe kuendelea na shughuli za chombo hicho kama ilivyopangwa.
Badala yake alichukua majina ya wabunge alioona kuwa walishiriki katika kelele hizo na kuwapeleka mbele ya Kamati ya Uongozi kwa ajili ya kujadiliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Ni kweli kwamba vurugu zinazofanywa bungeni hazifai na kwa kweli zinakwamisha shughuli za chombo hicho muhimu. Lakini tunadhani kuwa wabunge hao wamekosa njia nyingine ya kuhakikisha sauti zao zinasikika.
Kwa maana hiyo, badala ya kufikiria njia za kuwadhibiti, uongozi wa Bunge ujihoji sababu za uendeshaji wa chombo hicho kuanza kudorora na kuweka taswira mbaya kwa jamii.
Miswada hiyo ya sheria ni muhimu kwenye jamii kwa maana kuwa inapopitishwa inawagusa wananchi, wawakilishi wao hawana budi kuhakikisha kuwa mchakato wa kuipitisha ni lazima uwe wa mazingira ambayo ni muafaka kwa pande husika, yaani Serikali, wabunge na uongozi wa Bunge.
Kwenye semina hiyo, Serikali ilitakiwa itoe maelezo ya kina kuwashawishi wabunge kuwa kuna haja ya miswada hiyo kupitishwa sasa badala ya baadaye.
Lakini inaonekana Serikali ilishindwa na badala yake ikataka kutumika mbinu ya kutopokea mwongozo ili muswada usomwe na kupita hatua hiyo ili mambo yanayofuata yafanyike kama ilivyopangwa.
Huu si utaratibu mzuri na hautakiwi kutumika kwenye dunia ya sasa inayoendelea kujaa watu walioerevuka na wenye kuhoji kila kitu. Kinachotakiwa mbele ya jamii kama hiyo, ni majibu na maelezo ya kutosha kushawishi watu umuhimu wa jambo lililo mbele yao.


Wabunge kutoka upinzani wanajua kuwa kwa idadi ni wachache hivyo Serikali inapowasilisha jambo ni rahisi kwa wenzao wanaotoka chama kinachotawala, kulikubali hata kama halifai au lina kasoro. Ndiyo maana wameamua kutumia mbinu hiyo ya kelele.
Ni wazi kuwa uongozi wa Bunge utakapokuja na mbinu ya kuwadhibiti, wabunge hao pia watagundua mbinu ya kuondokana na kudhibitiwa na matokeo yake itakuwa ni vurugu.
Serikali na uongozi wa Bunge hawana budi kutafakari njia bora inayofaa kuitumia ambayo itaridhiwa na pande zote mbili kuliko utaratibu huu wa kuburuza wasioafiki jambo.
Demokrasia ni kuwapa wengi, lakini ni lazima hao wengi wawe wanafanya uamuzi ambao hauonekani kuwa na madhara kwa jamii. Na kwa maana hiyo, hata kama wengi wanaweza kupitisha jambo kwa idadi yao, ni vizuri kuwapo na ufafanuzi wa kutosha na baadaye kuridhia kukubaliana kutokubaliana kabla ya suala hilo kuingizwa ndani ya Bunge.

No comments:

Post a Comment