Friday, 3 July 2015

Chenge kubanwa Escrow kabla ya Oktoba 25.

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma limeeleza kuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, atahojiwa kuhusiana na kuhusika kwake katika sakata la fedha za akaunti iliyokuwa Benki Kuu (BoT) ya Tegeta Escrow kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Hatua hiyo ya Baraza inatarajiwa kuchukuliwa ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali zuio lake la Chenge la kutaka asihojiwe na baraza hilo kutokana na gawiwo la Sh. bilioni 1.6 kutoka akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
 
Taarifa za uhakika ambazo NIPASHE imezipata kutoka kwenye Baraza la Maadili zinasema kuwa kabla ya uchaguzi mkuu, Chenge na wenzake watatu ambao walikataa kuhojiwa na baraza hilo kuhusiana na mgawo wa Escrow sasa watahojiwa.
 
“Tume ilikuwa imepanga kuzungumza na waandishi wa habari leo (juzi), kuzungumzia suala hilo la kuhojiwa Chenge na wenzake waliokimbilia mahakamani, lakini imeshindikana kwa sababu baadhi ya maofisa wamesafiri kikazi,” alisema ofisa mmoja wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
 
Aliongeza: “Siwezi kusema ni lini atahojiwa (Chenge). Lakini taarifa itatolewa kwenye vyombo vya habari, kazi hii naamini itafanyika mapema hata kabla ya uchaguzi mkuu.”
 
Baadhi ya vigogo waliokataa kuhojiwa kutokana na kuwapo kwa zuio la mahakama ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philipo Saliboko na Kamishna Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo. Inaelezwa kuwa Saliboko alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4 na Appollo aligawiwa Sh. milioni 80.8.
 
Watuhumiwa waliohojiwa na kiasi walichodaiwa kupata kwenye mabano ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6); Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh. milioni 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7); majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh. milioni 404.25) na Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. milioni 40.4); na pia aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4.
 
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1993, kifungu cha (8), kinaeleza kuwa kati ya hatua ambazo viongozi wa umma wanaweza kuchukuliwa pale wanapobainika kukiuka sheria za utumishi wa umma ni pamoja na kuonywa, kushushwa cheo na kusimamishwa kazi.
 
Nyingine ni kufukuzwa kazi na kushauriwa kujiuzulu au kuwafikisha mahakamani baada ya kuwakuta na hatia.

No comments:

Post a Comment