Lowassa aliondoka hotelini hapo baada ya kukaa kikaoni kwa saa 1.38 (dakika 98). Aliagwa na viongozi mbalimbali wa Chadema.
Dar es Salaam. Katika dakika za mwishomwisho wakati wa mchakato wa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, habari za mmoja wa wagombea aliyekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro hicho, Edward Lowassa kwamba angeenguliwa zilivuma mno na kuibua swali la atakatwa hakatwi?
Sasa jibu la swali hilo la pili limepatikana. Ametoka na sasa ni rasmi kwamba atakuwa mgombea urais kupitia Ukawa.
Usiku wa kuamkia jana, Waziri Mkuu huyo wa zamani alihudhuria rasmi kikao cha Kamati Kuu ya Chadema katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutambulishwa pamoja na kujadiliana mikakati ya kuing’oa CCM madarakani.
Baada ya jana mchana, viongozi wa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia; Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walikutana na waandishi wa habari Dar es Salaam na kumkaribisha rasmi Lowassa kwenye umoja huo huku wakitumia muda mrefu kumsafisha dhidi ya tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akihusishwa nazo.
Atinga Kamati Kuu Chadema
Mwandishi wetu alimshuhudia mbunge huyo wa Monduli akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema juzi usiku.
Awali kikao hicho kilianza saa 9.30 alasiri katika Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam ambacho Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho walipata taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho ghafla Jumamosi kati ya saa nne na tano usiku kwa kupigiwa simu, lakini hawakuambiwa ukumbi wala madhumuni ya kikao hicho zaidi ya kuambiwa kuwa wanatakiwa wawepo Dar es Salaam siku hiyo.
Lowassa kikaoni
Lowassa alialikwa kuhudhuria kikao hicho na aliwasili katika lango la kuingia kwenye hoteli hiyo saa 3.02 usiku akiwa ndani ya gari jeusi aina ya Toyota Lexus, akiwa amevalia suti nyeusi na shati jeupe na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Baada ya hapo aliongozwa kuelekea katika Chumba cha Wageni Mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho wakiwamo Mbowe na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed.
Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3.20 usiku, walitoka na kuingia katika ukumbi ambao kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilikuwa kinafanyika.
Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4.58 usiku, alitoka katika ukumbi huo akisindikizwa na Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara), Profesa Abdallah Safari, Mohammed na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu ambao baadaye walirejea ukumbini kuendelea na kikao.
Habari za ndani
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinasema baada ya Lowassa kuwasili na kutambulishwa kwa wajumbe, alipewa nafasi ya kuzungumza.
Miongoni mwa mambo anayodaiwa kuwagusia ni pamoja na kashfa ya Richmond ambayo ilimlazimu kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008. Pia, inaelezwa kuwa wajumbe walitaka kujua utajiri wake na baada ya kupewa majibu, walijadiliana jinsi ya kuiangusha CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Ukawa wampokea, wamtetea
Saa 18 baada ya Lowassa kutambulishwa katika Kamati Kuu ya Chadema, viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari jana mchana na kumkaribisha rasmi katika harakati za kuing’oa CCM huku wakimsifia kuwa ni mchapakazi na mfuatiliaji wa karibu wa majukumu anayokabidhiwa.
Hatua hiyo Ukawa juu ya mtazamo kwa Lowassa ambaye amekuwa akituhumiwa kwa kashfa mbalimbali na viongozi hao wa upinzani, inaonyesha dhahiri kwamba ameshapata baraka za kujiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Wakati wa sakata la Richmond, viongozi wa upinzani walikuwa wakimponda kiongozi huyo na Dk Slaa aliwahi kumuweka kwenye orodha aliyoiita ‘list of shame’.
Viongozi hao walimtetea na kusema kuwa hakuna aliyewahi kuthibitisha tuhuma dhidi ya Lowassa na kuongeza kuwa mfumo wa CCM ndiyo wenye matatizo ya rushwa na si mtu.
Profesa Lipumba alisema suala la ufisadi ni mfumo na si la mtu mmojammoja... “Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi na chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM, kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na rushwa iliyopo.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015 lakini ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini, Tegeta Escrow Akaunti imetokea wakati gani, Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?
“Makaburu waliuana wakamfunga Mandela (Nelson) lakini alitoka gerezani na kukaa chini akazungumza nao, kipi cha ajabu? Msumbiji walipigana vita miaka 18, lakini walikubaliana, basi kama Lowassa anakubali kwamba Ukawa ni muhimu kwa Watanzania, amezinduka na kuona hata bora aende Ukawa akafanye mabadiliko.”
Alisema kwenye siasa hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu, bali kuna kudumu kwa hoja ambazo zina masilahi kwa Taifa... “Wacha Mzee Lowassa aje, tumechoka kuonewa.”
Dk Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, basi angekuwa amekwisha shtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.
“Hata Lowassa mwenyewe aliwahi kuuliza mwenye uthibitisho kuwa yeye ni fisadi ajitokeze na kumhukumu lakini mpaka leo hakuna aliyefanya hivyo.”
Alisema iwapo Lowassa ataamua kujiunga na Ukawa, wanamkaribisha kwa moyo wote kwani hakuna mwenye uthibitisho kuwa ni fisadi... “Mimi nasema sina wasiwasi, tunamkaribisha, sijaona ubaya wake.”
Mbatia alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo kandamizi na dhalimu wa CCM na kwamba watashirikiana naye kujenga Taifa imara na kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.
“Tunachukua fursa hii kipekee kumwalika Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, mheshimiwa Edward Lowassa ajiunge na Ukawa na tuko tayari kushirikiana naye kuhakikisha tunaiondoa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tunaamini mheshimiwa Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki. Ni mchapakazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa.”
Katika mkutano huo uliodumu kwa dakika 30, Mbatia alisema Ukawa inaamini kwa masilahi mapana ya Taifa inamhitaji kila Mtanzania ambaye yupo tayari kujiunga nao kuhakikisha Taifa linakuwa salama na lenye amani ya kweli ambayo msingi wake ni haki.
“Katika kutafakari kwa kina masilahi mapana ya Taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za Taifa kwa masilahi ya Watanzania wote.
“Viongozi wa aina hii hawawezi kuwa ndani ya CCM, maana mfumo wake haumpi kiongozi kutumia vipaji vyake au ubunifu wake katika kusimamia masilahi ya Taifa letu,” alisema.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kuhudhuriwa na wenyeviti na makatibu wote wa Ukawa kasoro Dk Slaa, Mbatia alisema: “Hatutakubali kunyamaza pale sauti zetu zinaponyamazishwa kwa lazima bila sababu. Tusikubali kunyimwa fursa ambazo tuna uwezo nazo… tuwe tayari kushiriki michakato ya kidemokrasia ya kuleta mabadiliko na kupata viongozi bora.”
Akizungumzia uamuzi wa kumpokea Lowassa, Profesa Lipumba alisema huo ni wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF na ambao uliafikiwa na Ukawa kwa ujumla.
“Msimamo wa chama chetu tangu kwenye Baraza Kuu ni mmoja, kuwa sisi kuendelea kushirikiana na Ukawa na tupate mgombea mmoja. Tuna wagombea wazuri wa urais lakini tunataka kupata mgombea mmoja atakayeweza kutusaidia kupata rais na kuiondoa CCM,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema hata tamko la jana la Ukawa limetokana na baraka za Baraza Kuu la Uongozi la hicho.
Alipoulizwa kuhusu chama chake kusuasua katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea wa urais kupitia Ukawa, Profesa Lipumba alisema chama hicho kilikuwa kinajadili suala hili kwa mujibu wa kanuni na taratibu zake.
“Wakati wote nilipochukua fomu, nilieleza wazi kuwa nipo tayari kugombea urais na nitagombea kupitia Ukawa na iwapo atatokea mgombea mwingine nitashirikiana naye na huu ndiyo msimamo hata wa chama,” alisema.
Kuhusu siku watakayomteua mgombea wa urais, Profesa Lipumba alisema mchakato huo utafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao kulingana na makubaliano ya Ukawa.
‘Ruksa’ kuchagua chama
Haji alisema Lowassa atachagua chama cha kujiunga nacho na huko atafuata taratibu iwapo atachagua kugombea nafasi ya urais.
“Kama atajiunga na chama A, B au C, basi chama hicho kitafuata taratibu zake, kama atajiunga na Chadema basi atafuata taratibu za huko lakini sisi vyama vingine tutamuunga mkono,” alisema.
Alipoulizwa iwapo Ukawa inakaribisha kwa sababu anaonekana kuwa na nguvu ya kuiangusha CCM, Haji alisema Ukawa ndiyo yenye uwezo wa kuiangusha CCM na mgombea wa umoja huo ndiye anayeshika bendera.
Mbowe kimya
Tofauti na mikutano ya nyuma ya umoja huo, Mbowe jana hakuzungumza chochote licha ya kuulizwa maswali moja kwa moja kuhusu kauli zake za awali zilizowahi kuonekana bayana kumshambulia Lowassa.
Hata alipofuatwa na wanahabari baada ya mkutano huo hakuzungumza chochote zaidi ya kueleza kuwa mambo yote yameelezwa kwa kina na wenzake.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Mohamed alipotakiwa kuthibitisha taarifa za Lowassa kushiriki vikao vya Chadema na kwamba ameshajiunga na chama chao, alisema kwa kifupi: “Sitaki kuzungumzia lolote juu ya hilo.”
Mgombea bado bado kwanza
Akizungumzia sababu za kuahirisha kumtangaza mgombea mara kwa mara ikiwamo jana, makamu mwenyekiti huyo wa Chadema alisema wamekubaliana vyama vimalize utaratibu wa vikao vya kikatiba ili kupata wagombea na baadaye wakae pamoja na Ukawa kupitisha jina moja na kumtangaza mgombea mmoja.
Alisema vyama vya siasa vinatakiwa kubadilika kulingana na hali halisi, hivyo kuna mambo ambayo yalitakiwa kufikiriwa zaidi kabla.
Pamoja na suala la kumpata mgombea wa urais, alisema bado kuna masuala yaliyo mezani yakiwamo kuachiana majimbo mapya 26 na yale ya Mkoa wa Dar es Salaam yaliyoonekana kuwa na mvutano mkubwa wa nani atayawakilisha.
No comments:
Post a Comment